1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa shirikisho Christian Wulff ajiuzulu

17 Februari 2012

Pendekezo la mwendesha mashtaka mkuu wa jiji la Hannover kutaka rais Wulff apokonywe kinga yake ya kutoandamwa ndilo lililomaliza udhia .

https://p.dw.com/p/14508
Rais Christian Wulff atangaza kujiuzuluPicha: dapd

Dhana za mwanzo za waendesha mashtaka wa mji wa Hannover ndizo zilizohitimisha wadhifa wa Christian Wulff kama rais wa shirikisho.Na hata kama kabla ya ushahidi kupatikana hata rais wa shirikisho hawezi kutiwa hatiani,lakini Christian Wulff aligeuka mzigo kwa wadhifa huo wa juu kabisa wa rais wa shirikisho ambao kwa kila hali unabidi uepushiwe madhara.Wakati wa kujizulu ulikuwa tayari umeshawadia,kama haujapindukia.Ni hatima ya kusikitisha ya Christian Wulff ambae tangu wiki kadhaa sasa amekuwa akijaribu kwa kila hali, kwa fasaha na upole kujitakasa na kashfa dhidi yake.Hakufanikiwa.Na bora hivyo kwasababi hali hiyo inatoa picha ya uhuru wa vyombo vya sheria na uandishi habari nchini Ujerumani.

Ripoti na mada ziligonga vichwa vya habari vya magazeti kuhusu jinsi alivyokuwa akipitisha likizo zake katika nyumba za ghali za fahari,jinsi alivyokuwa akiitika mialiko na kuchanganya masilahi ya kisiasa na kiuchumi,wakati alipokuwa waziri mkuu, kwa namna ambayo Christian Wulff amejikuta akinasa katika mkasa ambao hakuweza tena kujitoa hata kama alitaka.

Pendekezo la ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Hannover limekuja kubainisha uzito wa hali yeyewe hasa:hili si kosa dogo bali ni suala la kutathmini hali halisi namna ilivyo na kama kuna uwezekano wa kuandamwa kisheria.

Rücktritt Bundespräsident Christian Wulff
Christian na Bettina Wulff baada ya tangazo la kujiuzuluPicha: Reuters

Kipya lakini ni uamuzi wa kujiuzulu :Kwa mara ya kwanza katika historia ya shirikisho la jamhuri ya Ujerumani,inapenedekezwa kiongozi wa ngazi ya juu kabisa katika taifa hili apokonywe kinga yake.Hatua kama hiyo ina matokeo na madhara yake-mara nyingi wanasiasa hujiuzulu kabla ya hatua kama hiyo kupitishwa,kabla ya imani ya wananchi kwa wadhifa wake na chama chake cha kisiasa kuathirika.Christian Wulff angebidi afanye hivyo hivyo na pengine mapema.

Wadhifa wa rais wa shirikisho unategemea uaminifu na kutoelemea upande wowote mwenye kukabidhiwa wadhifa huo.Tofauti na nchi nyengine ambako madaraka ya wadhifa wa rais yanaweza kuenea hadi kushawishi maamuzi ya bunge au ya vyombo vya sheria,nchini Ujerumani madaraka ya rais wa shirikisho yana kikomo.Akiwa mwakilishi wa ngazi ya juu anaweza na anabidi kuhimiza na kuongoza mijadala katika jamii kuhusu mada muhimu za maadili.

Deutschland Schloß Bellevue in Berlin
Kasri la rais Schloß Bellevue mjini BerlinPicha: picture-alliance / dpa

Mpaka sasa bado idadi kubwa ya watu tangu ndani mpaka nje ya Ujerumani wanamuangalia Christian Wulff kama mhanga wa kampeni iliyoendeshwa na vyombo vya habari.Lakini kwa mtazamo wangu,katika kadhia hii ya Wulff vyombo vya habari vimefanya kile kinachowahusu tu nacho ni kuripoti,pale siasa na wanasiasa wanapojongeleana sana na makundi yenye masilahi mengine.Hivyo ndivyo wafanyavyo waandishi habari kote ulimwenguni na kwengineko waandishi hao wa habari wanatia hatarini maisha yaop kwasababu ya kutaka kufanya kazi yao.

Kwa Upande wa Christian Wulff,waandishi habari wamezusha mjadala kama kuna uwezekano wa kujifaidisha.Hiyo ni kazi yao.Na pendekezo la mwendesha mashtaka wa Hannover linaonyesha kuwa vyombo vya sheria ni huru humu nchini.

Ujerumani inasifiwa ulimwengu kote kwakuwa kila wakati tunapaza sauti kudai wengine pia waheshimu demokrasia,utawala unaofuata sheria na uhuru wa mtu kutoa maoni yake,kwa hivyo ni vyema kabisa ikiwa misingi hiyo inafuatwa kikamilifu humu nchini .

Mwandishi:Schaeffer,Ute/Hamidou Oummil

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman