1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa soka wa Uhispania agoma kujiuzulu kwa kosa la busu

25 Agosti 2023

Mkuu wa Shirikisho la Kandanda la Uhispania, Luis Rubiales, amekataa kujiuzulu kwa kitendo cha kumbusu mdomoni mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake, Jenni Hermoso, baada ya ushindi wa Kombe la Dunia la Wanawake.

https://p.dw.com/p/4VaXa
Fußball Spanien RFEF Präsident Luis Rubiales
Picha: RFEF/AFP

Katika mkutano wa dharura wa shirikisho hilo la kandanda uliofanyika siku ya Ijumaa (Agosti 25), Rubiales, mwenye umri wa miaka 46, alisema hatoachia nafasi yake.

Kiongozi huyo wa soka alisema shinikizo alilolipata wiki hii kutoka kwa wanasiasa na vilabu ni jaribio la "kutaka kumuangamiza" na atajitetea kwa kuwachukulia hatua watu hao.

Soma zaidi: FIFA kufungua kesi dhidi ya rais wa shirikisho la soka la Uhispania

Mkuu huyo wa kandanda Uhispania alisema busu lake kwa Hermoso lilikuwa kama kumbusu mtoto na haliwezi kufananishwa na udhalilishaji wa kingono.

Hatua yake ya kuendelea kung'ang'ania uongozi wa shirikisho hilo imewapelekea wanasiasa nchini humo, akiwemo Naibu wa Pili wa Waziri Mkuu, Yolanda Diaz, kutaka serikali ichukue hatua za haraka.