1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Salva Kiir ameteua wabunge 50 kutoka upande wa waasi

Admin.WagnerD8 Januari 2016

Rais wa Sudan Kusin Salva Kiir ameteua wabunge 50 kutoka vuguvugu la waasi na kukubali kugawanya nyadhifa za uwaziri na wapinzani wake kulingana na mkataba wa amani unaonuia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe .

https://p.dw.com/p/1Ha9o
Südsudan Riek Machar Salva Kiir
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Muller

Kwenye tangazo kupitia radio ya serikali ya nchi hiyo,Kiiir ametangaza uteuzi wa wabunge 50 waliopendekezwa na upande wa waasi.

Rais wa zamani wa Botswana Festus Mogae ambaye anaongoza tume ya pamoja ya kufuatilia na kutathmini iliyoundwa na jumuiya ya IGAD kuhakikisha mkataba huo unatekelezwa,amesema serikali itapewa nyadhifa 16 za uwaziri zikiwemo za ulinzi,usalama wa kitaifa,fedha na sheria huku waasi wakipewa nyadhifa 10 zikiwemo za mafuta na maswala ya kibinadamu.

Wafungwa wa zamani kupokea nyadhifa

Kundi la wanasiasa wenye ushawishi mkubwa lijulikanalo kama wafungwa wa zamani ambao walifungwa wakati mapigano yalipoanza lakini wakaachiliwa baadaye,watapokea wadhifa wa maswala ya nchi za kigeni na ule wa uchukuzi huku nyadhifa za maswala ya baraza la mawaziri na kilimo zikiendea vyama vingine vya kisiasa.

Pande zote mbili za serikali na waasi kwenye mzozo huo wa miaka miwili nchini Sudan Kusini zimelaumiwa kwa kuchochea mauaji ya kikabila,kusajili na kuwauwa watoto na kutenda visa vya unajisi,mateso na kuhamisha watu kwa nguvu ili kuwaondoa maeneo ya wapinzani wao.

Mzozo huo umesababisha mzozo wa kibinadamu huku watu milioni 2.3 wakilazimika kuhama makwao na wengine milioni 4.6 wakihitaji msaada wa chakula.Maelfu ya watu wameuawa na uchumi kuporomoka..

Watoto wanajeshi wakiwa na silaha Sudan Kusini
Watoto wanajeshi wakiwa na silaha Sudan KusiniPicha: picture-alliance/dpa/AA/S. Bol

Pande zote zimelaumiana kuvunja mikataba

Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar wameshutumiana kwa kuvunja mikataba ya amani lakini wanasema wangali wazingatia makubaliano ya tarehe 26 mwezi Agosti,licha ya kushindwa kuafikia tarehe za mwisho zilizowekwa.

Chini ya makubaliano hayo Machar anastahili kuchukua wadhifa wa makamu wa Rais,wadhifa aliofutwa mwaka 2013.Kiongozi huyo wa waasi hadi sasa hajasafiri hadi Juba kuchukua nafasi hiyo.

Hakuna muda uliyowekwa wa lini mawaziri watateuliwa na kuchukuwa nyadhifa hizo.Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza mwei Disemba 2013 wakati Kiir alipomlaumu Machar kwa kupanga mapinduzi,hatua iliyosababisha mauwaji ya kilipiza kisasi ambayo yameigawanya kikabila nchi hiyo masikini.

Serikali hiyo ya muungano,itadumu kwa muda wa miaka 3 kabla ya uchaguzi kufanyika na itakuwa na wizara 30.

Wachambuzi wamepongeza hatua hiyo lakini wakaonya kuwa maswala mengi muhimu kwenye makubaliano ya amani hayajashughulikiwa.

Mwezi uliopita Kiir alifutilia mbali mfumo wa zamani wa majimbo 10,na kuunda maeneo mapya 28 na hivyo kuenda kinyume na mkataba wa kugawanya mamlaka.

Mapigano yanaendelea na mzozo huo sasa unahusisha makundi kadhaa ya wapiganaji ambayo hayazingatii mikataba iliyoandikwa ya amani,huku yakiongozwa na ajenda za maeneo yao na mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Mwandishi:Bernard Maranga/AFP/AP

Mhariri:Iddi Ssessanga