1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Tanzania avunja Baraza la Mawaziri

8 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D4Cv

DAR-ES-SALAAM:

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete amevunja Baraza la Mawaziri baada ya kukubali kujiuzulu kwa waziri wake mkuu na mawaziri wengine wawili kufuatia kashfa ya rushwa.Siku ya Alkhamisi,Waziri Mkuu Edward Lowassa alitangaza bungeni kuwa ameamua kujiuzulu baada ya hadhi yake kutiwa doa kwa ripoti inayohusika na utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Kimarekani Richmond kuzalisha umeme nchini Tanzania.Waziri wa Nishati Nazir Karamagi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ibrahim Msabaha aliekuwa na wadhifa wa nishati hadi Oktoba 2006 vile vile wametoa barua zao za kujiuzulu.Baadae ofisi ya Rais ilitangaza kuwa Kikwete amekubali kujuzulu kwa viongozi hao na bunge likavunjwa.

Ripoti ya tume ya bunge iliyochunguza kandarasi ya kuzalisha umeme imesema, waziri mkuu na mawaziri wengine wawili na hata maafisa kadhaa waliingilia kati utoaji wa zabuni ili kuipendelea kampuni hiyo ya Kimarekani.Kandarasi hiyo imehusika na uzalishaji wa umeme wa dharura nchini Tanzania panopotokea hali ya ukame.Lowassa akilalamika kuwa hakutendewa haki amesema hakupewa nafasi ya kujieleza.

Edward Lowassa alishika wadhifa wa uwaziri mkuu Desemba mwaka 2005.Kashfa hiyo ya kisiasa isiyo na mfano,imeibuka juma moja kabla ya ziara inayotazamiwa kufanywa na Rais wa Marekani George W.Bush nchini Tanzania.