1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Uganda akamilisha ziara yake nchini Rwanda

1 Agosti 2011

Serikali za Rwanda na Uganda zimekubaliana kushirikiana kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo. Maazimio hayo yamefikiwa na pande mbili kwenye kilele cha ziara ya siku nne ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni nchini Rwanda.

https://p.dw.com/p/128gS
Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: DW/Schlindwein

Ziara ya Rais Museveni licha ya kujikita katika ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, imekuwa ikitazamwa na wadadisi kama inayofungua ukurasa mpya wa uhusiano wa nchi hizo ambao ulikuwa umedorora kwa muongo mmoja uliopita.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Louise Mushikiwabo ndiye aliyelisoma tangazo la pande mbili lililotiwa saini na mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda na Uganda. Tangazo hilo linaainisha sehemu ambazo nchi hizo zitashirikiana, ikiwa ni pamoja na uchumi, sayansi na teknolojia na hifadhi ya mazingira. Punde tu marais hao wakaanza mazungumzo na waandishi wa habari.

Madai ya mvutano kati ya Rwanda wa Uganda yapuuzwa

Waandishi wa habari walikuwa na shauku ya kujua ukweli wa jitihada za marais hao kuondoa tofauti zao ambazo zimekuwa zikiendelea ingawa chini kwa chini kwa takribani muongo mmoja uliopita. Hata hivyo marais wote walionekana kupuuza ikiwa kumekuwepo na mgogoro wowote, huku wakisisitiza kuwa nchi za Rwanda na Uganda zimekuwa na mafungamano ya kihistoria.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ametoa mfano kama kuhakikisha ukweli huo akisema kwamba watu wa eneo la maziwa makuu ni ndugu. Akaongeza kusema, "Mauaji yalipoanza nchini Rwanda miaka ya 59 Wanyarwanda hawakukimbilia Paris wala Brussels lakini walikimbilia Uganda,Tanzania, Kongo na nchi nyingine jirani. Wakati Iddi Amin akifanya mauaji Uganda mimi sikukimbilia London nilikimbilia Tanzania."

Tangu alipowasili nchini siku ya Ijumaa jioni Rais Yoweri Museveni amekuwa akitembelea sehemu mbalimbali za kimaendeleo, na kauli yake imekuwa kukisifu chama tawala cha Rwanda, RPF ambacho alikuwa miongoni mwa watu waliokiunga mkono wakati wa harakati zake za kusimamisha mauaji ya kimbari na kutwaa madaraka mjini Kigali mwaka 1994.

Ruanda Präsidentschaftswahl 2010 Afrika Kigali Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: picture-alliance/dpa

Ziara muhimu kwa pande zote

Kwa upande wake Rais Paul Kagame akasema ziara ya rais Museveni ilikuwa muhimu si kwa viongozi wa Rwanda lakini pia kwa wananchi wa nchi zote kwa kufafanua kuwa hii ni ishara ya uhusiano na ujirani mwema.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Yoweri Museveni kufanya ziara ya siku nyingi nchini Rwanda, mwaka 2009 alipokuja kutunukiwa nishani za heshima hakulala alikuja na kuondoka na wakati huo wengi walihisi kweli kulikuwepo na matatizo.

Mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda na Uganda wamesema kwa pamoja kuwa madai kuwa kuna sintofahamu baina ya nchi hizi mbili ni porojo tupu na kwamba hata kama kungekuwepo na matatizo basi nchi hizo haziwezi kushindwa kuyatatua. Rais Museveni ameondoka jioni hii kuelekea Kampala kwa kuacha mwaliko kwa rais Paul Kagame ambaye amekubali bila hata hivyo kutaja ni wakati gani ataizuru Uganda.

Mwandishi: Sylvanus Karemera

Mhariri: Josephat Charo