1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ujerumani aendelea na ziara yake Tanzania

4 Februari 2015

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani anaendelea na ziara yake nchini Tanzania, ambapo jana alikula chakula cha jioni alichoandaliwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwenye ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.

https://p.dw.com/p/1EVDN
Rais Gauck akigonganisha glasi na mkewe, Daniela Schadt na Rais Kikwete
Rais Gauck akigonganisha glasi na mkewe, Daniela Schadt na Rais KikwetePicha: DW / Khelef Mohammed

Pamoja na mambo mengine, Rais Gauck ameyasifu maendeleo ya kisiasa na kiuchumi ya Tanzania lakini alisema kwamba bado mengi yanahitajika kufanyika kuwawezesha wananchi wa kawaida, ambao ndio wanaobeba machungu yote ya kisiasa na kiuchumi.

Rais Gauck amekamilisha sehemu hii ya kwanza muhimu ya ziara yake kwenye mji mkuu wa kibiashara, Dar es Salaam, kwa kurejelea mtazamo wa Ujerumani kwa Tanzania, kama taifa la Afrika ya Mashariki linaloinukia kwa kasi kwenye ukuwaji wa uchumi, hatua ambayo amesema inachangiwa sana na uwepo wa amani na utulivu wa kisiasa kwenye taifa ambalo limekuwa kigezo kote Afrika.

''Tanzania ni sehemu ya soko lenye watu milioni 145 la Afrika ya Mashariki. Soko hili la pamoja sio tu linaimarisha fursa za ukuwaji wa uchumi na hali ya maisha, bali ushirikiano huu unafungua pia milango ya fursa za amani na utulivu kwa eneo hili zima, mambo ambayo ni msingi wa mustakabali mwema unaotakiwa na wanaume, wanawake na watoto barani Afrika,'' alisema Gauck,

Rais Joachim Gauck
Rais Joachim GauckPicha: DW / Khelef Mohammed

Kwa upande wake, mwenyeji wa Rais Gauck, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania aliitolea tena wito Ujerumani kuimarisha uwekezaji wake kwenye sekta kadhaa zinazokuwa nchini Tanzania, hasa soko la utalii, ambalo tayari Ujerumani imeonesha muelekeo mzuri.

''Ujerumani ni chanzo kikuu cha watalii wanaoingia Tanzania. Kama ambavyo utaona kwenye ziara yako ya Zanzibar, Arusha na Serengeti, tuna fursa nyingi. Hivyo tunawakaribisha wale wenye nia ya kuwekeza kwenye utalii kufanya hivyo,'' alifafanua Rais Kikwete.

Nchi hizi mbili zina ushirikiano wa muda mrefu

Tanzania na Ujerumani zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu kupitia miradi inayosimamiwa na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Ujerumani, GIZ, ambayo inajumuisha sekta za afya, maji na nishati, lakini kwa siku za hivi karibuni sera za nje za mataifa hayo zimejikita zaidi kwenye utumiaji wa fursa za kiuchumi zinazopatikana pande zote mbili.

Kabla ya hafla hiyo, ujumbe wa wafanyabiashara uliombatana na Rais Gauck ulikuwa na mazungumzo na wafanyabiashara wenzao wa Tanzania kwenye ofisi za ubalozi wa Ujerumani jijini Dar es Salaam, kwa lengo la pande hizo mbili kuangalia maeneo ya ushirikiano.

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya KikwetePicha: DW / Khelef Mohammed

Kwa upande mwengine, mke wa Rais Gauck, Mama Daniela Schadt aliongoza ujumbe mwengine kutembelea kituo cha matibabu ya ugonjwa wa fistula na ulemavu mwingine wa viungo kando kidogo ya kitovu cha jiji la Dar es Salaam, CCBRT, akiwa na mwenyeji wake, mke wa Rais Kikwete, Mama Salma Kikwete:

Mama Kikwete alisema, ''Ujerumani na Tanzania ni washirika kwenye hii hospitali ya CCBRT. Ni hospitali maalum kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania wenye mahitaji maalum. Lakini kikubwa kuna tatizo la fistula, ni ugonjwa ambao unamdhalilisha mwanamke. Wanawake wengi sasa wamepata matumaini mapya kwa sababu wanatibiwa.''

Kwaya ya jeshi la Polisi nchini Tanzania, ilitumbuiza katika hafla hiyo ya chakula cha jioni iliyohudhuriwa pia na viongozi kadhaa wa Tanzania, akiwemo makamu wa Rais, Dk. Gharib Mohamed Bilal, Jaji Mkuu Mohammed Chande Othman, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, Rais wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, na ujumbe ulioambatana na Rais Gauck kwenye ziara hii.

Mke wa Gauck, Daniela Schadt akiwa na Mama Salma Kikwete, katika hospitali ya CCBRT
Mke wa Gauck, Daniela Schadt akiwa na Mama Salma Kikwete, katika hospitali ya CCBRTPicha: DW / Khelef Mohammed

Hivi leo ziara ya Rais Gauck inaingia sehemu ya pili kwa kutembelea visiwani Zanzibar, ambako atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Ali Mohamed Shein, na baadaye kukutana na wawakilishi wa taasisi za kidini, kabla ya baadaye jioni kuelekea Arusha.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW
Mhariri: Grace Patricia Kabogo