1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ujerumani Köhler nchini Vietnam

21 Mei 2007

Rais wa Ujerumani Horst Köhler,anaendelea leo na ziara yake ya Asia kwa mazungumzo nchini Vietnam.Kesho, anaelekea China.

https://p.dw.com/p/CHE3

Rais Horst Kohler wa Ujerumani, yuko kwenye ziara ya wiki moja barani Asia:Kituo chake cha kwanza ni Vietnam.Licha ya vikwazo vya kisiasa na kukanyagwa haki za binadamu ,uchumi wa Vietnam unazidi kukua .

Rais Horst Kohler wa Ujerumani, aliwasili mjini Hanoi, mji mkuu wa Vietnam jana .Ajenda kuu ya mazungumzo yake na viongozi wa Vietnam ni raslimali,haki za binadamu na badiliko la hali ya hewa.

Rais Kohler ambae ni kama mkuu wa dola tu,alipowasili Hanoi hapo jana alikutana na rais Nguyen Minh Triet na baadae akawa na mazungumzo na waziri mkuu Nguyen Tan Dung.

Rais Kohler aliongoza sherehe na wizara ya elimu ya Vietnam kuanzisha mafunzo ya lugha ya kijerumani katika shule za Vietnam pamoja na kuasisiwa kwa chuo kikuu cha pamoja baina ya Vietnam na Ujerumani.

Hamu kuu ya Ujerumani nchini Vietnam ni kuhimiza humo nchini mageuzi na kuona Vietnam inaregeza vikwazo vyake vya kibiashara kuhimiza raslimali kutoka kwa wanabiashara wa Ujerumani ili kuharakisha zaidi ukuaji wake wa kiuchumi.

Leo hii,rais wa Ujerumani ana miadi na Katibu-mkuu wa chama cha Kikoministi Nong Duc Manh na hapo yamkini akalizusha swali nyeti la kukiukwa nchini Vietnam haki za binadamu.

Kwani, serikali ya Ujerumani imeingiwa na wasi wasi na msimamo wa serikali ya Vietnam kwa wapinzani huku zaidi ya darzeni 1 wakiwa wametiwa ndani mwaka huu pekee.

Vietnam ya kikoministi ina usuhuba mwema na Ujerumani kutokana na ushirika wake na iliokua Ujerumani mashariki (GDR).wakuu hadi 40 wa kivietnam wanazungumza kijerumani baada ya kuwa walihudhuria masomo katika vyuo vikuu vya Ujerumani Mashariki.

Isitoshe miongoni mwa wakaazi milioni 84 wa Vietnam ,laki mopja na nusu waliishi Ujeruzmani na Ujerumani imeonesha hamu ya kupalilia uhusiano mwema na kizazti cha sasa cha wanafunzi hao wa zamani.

Kwanini lakini Vietnam imekomea bado milango yake kuruhusu ushawishi kutoka nje,makamo wa waziri-mkuu wake Wu Quan anaeleza:

“Tumejionea matokeo katika nchi nyengine na tunafuata mkondo wetu wenyewe kuelekea demokrasia.Kubadili mifumo yetu kutaleta tu hali ya wasi wasi.”

Kwamba wabunge wapya wangepigania Vietnam ifungue milango yake ya kisiasa si jambo la kutarajia.Kwahivyo, rais Horst Köhler wa Ujerumani hataweza kubadili mengi katika mazungumzo yake ya leo na Katibu mkuu wa chama cha Kikoministi cha Vietnam.

Kesho, rais Kohler,ataondoka Hanoi kuelekea nchi jirani ya Jamhuri ya Watu wa China.