1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ukraine akataa kuurefusha muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano

Admin.WagnerD1 Julai 2014

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amesema majeshi ya serikali yataanza tena opresheni za kukabiliana na waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki mwa Ukraine baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kumalizika

https://p.dw.com/p/1CTGu
Picha: Reuters

Rais Petro Poroshenko ambaye anaishutumu Urusi kwa kuuchochea mzozo huo wa mashariki mwa Ukraine amepuuzilia mbali juhudi za Urusi za kuutuliza mzozo huo na kuwashutumu waasi hao wanaoungwa mkono na Urusi kwa kushindwa kuyaheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano au kuuzingatia mpango wake wa kutafuta amani.

Katika hotuba aliyoitoa kwa taifa hapo jana usiku,Poroshenko ameapa kukabiliana na waasi hao ili kuiokoa Ukraine kutoka mikononi mwa waasi na kuongeza kuwa uamuzi wa kutorefusha makubaliano ya kusitisha mapigano ni ujumbe kwa magaidi na wanamgambo kuwa watakabiliwa ipasavyo.

Majeshi ya Ukraine yanaripotiwa hii leo kuanzisha mashambulizi dhidi ya waasi hao mashariki mwa Ukraine licha ya juhudi za dakika za mwisho mwisho za viongozi wa Ulaya hapo jana kutafuta kuuongeza muda wa kusitisha mapigano.

Mapigano yazuka upya mashariki mwa Ukraine

Spika wa bunge la Ukraine Oleksandr Turchynov ameliambia bunge hii leo kuwa awamu nyingine ya opresheni za kijeshi imerejea katika ngome za waasi hao.

Spika wa bunge la Ukraine Oleksander Turchynov
Spika wa bunge la Ukraine Oleksander TurchynovPicha: Reuters

Rais wa Ufaransa Francois Hollande,Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,Rais wa Urusi Vladimir Putin na Poroshenko jana walifanya mazungumzo ya pande nne kwa siku ya tano mfululizo kutafuta njia muafaka ya angalau kuupunguza mzozo huo wa Ukraine.

Lakini licha ya juhudi hizo za kidiplomasia, mapigano yameripotiwa leo katika eneo hilo la mashariki.Raia wanne wameuawa katika mashambulizi ya asubuhi ambayo pia yamewajeruhi watu wengine watano na kufikisha idadi ya waliouawa katika mzozo huo tangu uanze kufika 450

Viongozi wa Ulaya watazidisha juhudi za kidiplomasia

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius amesema Ufaransa na Ujerumani hazitalegeza kamba katika juhudi za kutafuta amani nchini Ukraine na kuongeza kuwa kile wanachotafuta hivi sasa ni suluhu la muda mrefu la kusitisha mapigano,Ukraine kuwa na nguvu za kulinda mipaka yake na pia suala la kuhakikisha waliotekwa nyara wanaachiwa huru.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

Urusi kwa upande wake imesema uamuzi wa Poroshenko wa kutorefusha muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano umetokana na shinikizo kutoka nje na kwamba imesikitishwa na uamuzi huo huku ikizitaka nchi za kigeni kukoma kuitumia Ukraine kama chambo cha kufanya siasa za udhibiti wa kanda.

Mbunge wa Ujerumani Nobert Roettgen ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu masuala ya kigeni amekiambia kituo cha redio cha Ujerumani kuwa Umoja wa Ulaya leo unatarajiwa kufanya uamuzi wa kuiwekea Urusi vikwazo zaidi kwa kuendelea kuuchochea mzozo wa mashariki mwa Ukraine.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp/ap

Mhariri:Yusuf Saumu