1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Urusi afanya mkutano wa mwaka

1 Februari 2007

Rais Vladmir Puttin wa Urusi leo hii anakutana na waandishi wa habari mjini Moskow, kujibu maswali mbali mbali katika mkutano wa mwaka na waandishi habari.

https://p.dw.com/p/CHKy
Rais Vladmir Puttin wa Urusi
Rais Vladmir Puttin wa UrusiPicha: AP

Katika mkutano huo mkubwa wa mwaka rais Puttin anakutana na zaidi ya waandishi habari 1,100 kutoka kote ulimwenguni.

Katika hotuba yake ya ufunguzi rais Vladmir Puttin amesema..Urusi haitumii nafasi ya uchumi wake unaokuwa na utajiri wa nchi yake kwa ajili ya kujinufaisha katika maswala yake ya siasa nje.

Kile kinachojitokeza ni kuwa rais Puttin amejipanga kutetea hadhi ya nchi yake na hasa uhusiano wake wa nje ambao unazidi kudidimia siku hadi siku.

Mkutano huo unaonyeshwa moja moja katika runinga ya taifa kutoka ikulu ya Kremlin mjini Moskow.

Mkutano kama huo wa mwaka jana ulichukuwa takriban saa tatu na nusu na maoni ya wadadisi, wanasema kwamba huenda rais Puttin huandaa mikutano aina hii ili kujionyesha kuwa ana uwezo mkubwa wa kuyakabili maswali yenye utata kutoka kwa waandishi habari na pia ufahamu wake mkubwa wa kuyakabili maswala yanayohusiana na takwimu.

Swala jingine ambalo kwamba litapewa kipaumbele na rais Puttin ni swala ni kuhusu kampeni ya kuongezwa bei ya gesi dhidi ya mataifa jirani wa Urusi na pia kukatizwa huduma za nguvu za umeme mara kwa mara katika nchi za umoja wa ulaya kwa mfano wakati kulipotokea mikwaruzano kati ya Urusi na nchi za Belarus na Ukraine.

Tukumbuke pia hadhi ya rais Puttin imeathirika kiasi cha haja kufuatia vifo vya wapinzani wa serikali ya Kremlin katika mwaka uliopita wa 2006, kwa mfano mwandishi habari za kisiasa Anna Politkovskaya na aliyekuwa kachero Alexander Litvinenko miongoni mwa wengine.

Vile vile rais Puttin anatazamiwa kuzungumzia hali ya kiuchumi au kukua kwa uchumi wa nchi yake na pia hali ya utulivu iliyodumishwa katika jimbo la kaskazini la Caucasus pamoja na Chechniya yakiwemo pia majimbo mengine yanayokaliwa na waislamu.

Katika mkutano huo jambo jingine ambalo rais Puttin anatazamiwa kulizungumzia ni pamoja na lawama za Marekani dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran unaosimamiwa na Urusi na wakati huo huo kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Juu ya yote hayo rais Puttin pia anatarajiwa kueleza mpango wake wa baadae kutokana na kwamba kipindi chake cha utawala kinakamilika mwaka ujao je anapanga kumuunga nani mkono katika kuchukua wadhfa wa kuiongoza Urusi baada ya yeye kung’atuka madarakani?.

Mkutano huu wa mwaka na waandishi wa habari umepokelewa kama ufunguzi muhimu katika jarida la kisiasa nchini Urusi, kwani uchaguzi wa bunge umepangwa kufanyika tarehe 2 mwezi Desemba mwaka huu na kufuatiwa na uchaguzi wa rais hapo Machi tarehe 2 mwaka 2008.