1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Yemen aahidi kujibu mashambulizi

4 Juni 2011

Yemen inaelekea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati Rais Ali Abdullah Saleh leo akiahidi kujibu mashambulizi baada ya kujeruhiwa kwa maroketi yaliyofyatuliwa na wapinzani wa kundi la makabila kwenye Ikulu.

https://p.dw.com/p/11UFE
Rais wa Yemen, Ali Abdullah SalehPicha: dapd

Rais Saleh ambaye kwa miezi kadhaa amekuwa anakabiliwa na upinzani dhidi ya utawala wake, alijeruhiwa kidogo kisogoni. Serikali ya Rais Saleh inalishutumu kundi hilo la kikabila linaloongozwa na Sheikh Sadiq al-Ahmar kuhusika na shambulio hilo.

Jemen Protest gegen Regierung
Kiongozi wa kikabila Yemen, Sadiq al-Ahmar (Kulia) akiwa na afisa wa polisi anayeipinga serikaliPicha: picture-alliance/dpa

Katika taarifa iliyotolewa jana jioni, Rais Saleh ambaye anatibiwa katika hospitali ya wizara ya ulinzi mjini Sanaa, amesema anaendelea vizuri na kuongeza kusema kuwa mashambulio hayo yamewaua watu saba.

Wakati huo huo, Ujerumani leo imeamuru kufungwa kwa ubalozi wake nchini Yemen na kurudishwa haraka kwa wafanyakazi wake kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje imesema japokuwa mapigano kwenye mji mkuu wa Sanaa hayawalengi raia wa kigeni, hatari iliyopo ndiyo imeisababisha wizara hiyo kuchukua uamuzi huo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)
Mhariri: Mohamed Dahman