1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Yemen anaendelea kupata nafuu

6 Juni 2011

Rais wa Yemen, Ali Abdullah Saleh anaendelea kupata nafuu kutokana na upasuaji aliofanyiwa nchini Saudi Arabia wa kuondoa risasi kwenye kifua chake.

https://p.dw.com/p/11Uvx
Rais wa Yemen, Ali Abdullah SalehPicha: dapd

Waandamanaji wanaotabiri kutokuwepo kwa Rais Saleh kama ishara kwamba utawala wake ulikuwa ukidhoofika, walisherehekea katika mitaa ya mji mkuu wa Sanaa, ambako wamekuwa wakifanya maandamano ya kuipinga serikali tangu mwezi Januari, mwaka huu.

Rais Saleh alijeruhiwa Ijumaa iliyopita baada ya ikulu yake kushambuliwa kwa maroketi. Katika shambulio hilo watu saba waliuawa na washauri wake wa karibu walijeruhiwa. Rais Saleh anatibiwa katika hospitali ya Riyadh.

Suala muhimu katika siku zijazo litakuwa taarifa zozote kuhusu hali ya Rais Saleh na ishara yoyote kutoka Saudi Arabia iwapo ataweza kurejea Yemen au iwapo Saudi Arabia itaweka shinikizo kwa kiongozi huyo kujiuzulu. Machafuko yaliongezeka nchini Yemen baada ya Rais Saleh kukataa kusaini makubaliano ya kuondoka madarakani, ambayo yalisimamiwa na mataifa jirani ya Ghuba.