1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Brazil afunguliwa mashitaka

10 Machi 2016

Waendesha mashitaka nchini Brazil wamemfungulia mashitaka rais wa zamani wa nchi hiyo Luiz Inacio Lula da Silva, kwa kujipatia fedha kwa njia haramu.

https://p.dw.com/p/1IAa8
Brasilien ehemaliger Präsident Luiz Inacio Lula da Silva
Rais wa zamani wa Brazil Luiz Inacio Lula da SilvaPicha: Reuters/R. Moraes

Shutuma hizo zilizowasilishwa na waendesha mashitaka wa jimbo la Sao Paulo, zinatokana na madai kwamba kiongozi huyo amekuwa akificha umiliki wake wa nyumba iliyoko katika ufukwe wa bahari wa mji wa Guaruja.

Silva anakanusha kuwa anamiliki nyumba hiyo kisiri, ambayo inasemekana inamilikiwa na kampuni moja ya ujenzi ya OAS inayohusishwa pia na sakata moja kubwa katika kampuni ya mafuta ya seriklai ya Petrobras. Wiki iliyopita Silva alikamatwa na kuhojiwa na polisi, huku nyumba yake ikiwa imevamia kwa kufanyiwa uchunguzi.

Mashitaka aliyofunguliwa Silva leo hii, bado yanahitaji kuidhinishwa na jaji. Katika taarifa ya kiongozi huyo wa zamani wa Brazil, amesema waendesha mashitaka wa jimbo hilo la Sao Paulo hawana mamalaka ya kumfanyia uchunguzi.

Ijumaa iliyopita wachunguzi wanaoyashughulikia mashitaka dhidi ya kiongozi huyo, walisema wanaendelea kuchunguza iwapo kiongozi huyo alitumia wadhifa wake wa kisiasa katika kuzifanyia ukarabati nyumba mbili moja wapo ikiwa hiyo iliyopo ufukweni

Demonstration Anhänger von Luiz Inacio Lula da Silva
Maandamano dhidi ya Luiz Inacio Lula da SilvaPicha: Reuters/P. Whitaker

Silva akanusha mashitaka

Nyumba zote mbili zinadaiwa kuwa zilifanyiwa ukarabati mkubwa uliolipiwa na kampuni za ujenzi ambazo kwa miongo kadhaa zimekuwa zikifanya kazi pamoja na serikali ya shirikisho ya Brazil. Kampuni ambazo zimejumuishwa katikati ya sakata la bilioni 2, linaloihusisha pia kampuni ya mafuta ya seriklai ya Petrobras.

Hata hivyo Silva alikanusha madai hayo, kwa kusema nyumba ya ufukweni aliwahi kuitembelea mara mbili lakini haimiliki. Halikadhalika alidai nyumba hiyo ya pili inamilikiwa na rafiki yake.

Maafisa wanaohusika na uchunguzi huwo wanatarajiwa kufanya mkutano na waandishi habari kesho.

Silva aliwahi kuwa rais wa Brazil kuanzia mwaka 2003 hadi 2010. Licha ya kukabiliana na kashfa ya uibaji kura, iliyomuangusha mkuu wake wa wafanyakazi na viongozi wengineo, rais huyo wa zamani aliondoka madarakani akiwa bado ana umaarufu mkubwa miongoni mwa wananchi. Halikadhalika kiongozi aliyemchagua kumpokea uongozi ambaye ndiyo raisi wa sasa wa nchi hiyo Dilma Rousseff alifanikiwa kiurahisi kushinda katika uchaguzi uliomuweka madarakani.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape
Mhariri:Josephat Charo