1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Iran Rafsanjani afariki dunia

Iddi Ssessanga
8 Januari 2017

Rais wa zamani wa Iran Akbar Hasehmi Rafsanjani, amefariki baada ya kuugua maradhi ya moyo. Rafsanjani aliekuwa na umri wa miaka 82 alikuwa mtu muhimu katika kuasisiwa kwa Jamhuri hiyo ya Kiislamu mnamo mwaka 1979.

https://p.dw.com/p/2VUCJ
Iran Akbar Haschemi Rafsandschani
Picha: Getty Images/AFP//A. Kenare

Rafsanjani alikuwa malezawa katika hospitali ya Shohadaa kaskazini mwa mji mkuu wa Iran Tehran, mmoja wa ndugu zake Hossein Marashi alinukuliwa na mashirika ya habari akisema. Rafsanjani alihudumu kama rais kati ya mwaka 1989 na 1997.

Alishindwa vibaya katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2005 na mgombea mwenye msimamo mkali Mahmoud Ahmadinejad, katika kile kilichoonekana kama  upinzani wa wahafidhina.

Lakini badala ya kujitenga na siasa kutokana na fedheha hiyo, alisalia katika nafasi ya kuonekana na watu, akiibuka kama mwanasiasa mwenye msimamo wa wastani kupambana na wahafidhina wenye msimamo mkali waliomzunguka Ahmadinejad, ambaye chini ya uongozi wake uhusiano wa Iran na nchi za Magharibi ulishuka kwa kiwango kikubwa.

Katika miaka ya karibuni, ushawishi wake ndani ya taasisi za serikali ulikuwa umepungua. Mnamo mwaka 2013 ugombea wake wa nafasi ya rais ulikataliwa kwa sababu ya umri wake uliokuwa umekwenda.

Mwaka uliofuata, alitoa uungaji mkono muhimu kwa mshindi wa uchaguzi huo, Hassan Rouhani, mfuasi wa siasa za wastani ambaye walikuwa na urafiki wa karibu.

Alishikilia uwenyekiti wa chombo kikuu cha utatuzi wa migogoro cha Iran, Baraza la ushauri, tangu mwaka 1990, wakati alipoteuliwa na kiongozi wa juu Ayatollah Ali Khamenei.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape

Mhariri: John Juma