1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Wulff wa Ujerumani ajiuzulu

17 Februari 2012

Rais wa Ujerumani Christian Wulff amejiuzulu. Kiongozi huyo amekuwa akikabiliwa na kashfa ya kupokea mkopo wa fedha katika njia ambazo si halali, na uungwaji mkono kwake umeshuka sana.

https://p.dw.com/p/144i9
Rais Christian Wulff akitoa tangazo la kujiuzulu
Rais Christian Wulff akitoa tangazo la kujiuzuluPicha: Reuters

Katika hotuba yake muda mfupi uliopita, Christian Wulff ameshukuru kwa muda aliokaa madarakani kama Rais wa Ujerumani, akaongeza lakini kwamba ofisi hiyo kwa sasa inahitaji mtu mwenye hadhi bora na anayeaminiwa na wananchi. Amesema kwa sasa yeye hana hadhi hiyo.

Tangazo lake la kujiuzulu limekuja saa chache baada ya Mwendeshamashtaka mkuu kusema anaazimia kuomba kinga ya bwana Rais Wulff iondolewe ili uchunguzi ufanywe juu ya shutuma zinazomkabili.

Kuondolewa Kinga

Habari kwamba mwendeshamashtaka mkuu wa Serikali alikuwa ameomba kinga ya Rais iondolewe ili aweze kuchunguzwa imekuwa kama mlipuko wa bomu katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin. Mwendeshamashtaka mkuuu alikuwa amesema kuwa uchunguzi wa makini umedhihirika kwamba kuna vigezo vya kutosha na vya kuaminika, kuonyesha kwamba Rais Christian Wulff alitumia vibaya madaraka yake alipokuwa waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony

Utaratibu wa kufanya hivyo unaeleweka; Mwendeshamshtaka mkuu humwandikia barua waziri wa sheria kuomba kinga hiyo iondolewe, na waziri huwasilisha barua hiyo bungeni. Baada ya ombi hilo kuwasili bungeni, Rais wa Bunge, Norbert Lammert anawajibika kuiarifu kamati ya kinga bungeni. Kamati hiyo hukutana na kutafakari ombi hilo na kisha kutoa mapendekezo yao mbele ya kikao cha bunge zima.

Kupoteza imani ya wanasiasa

Hadi sasa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekuwa akiunga mkono uamuzi wa Rais Wulff kukataa kujiuzulu. Lakini shinikizo limekuwa likikua kutoka pande mbali mbali kumtaka Merkel kubadili mawazo yake.

Katika tamko lake kufuatia azma ya mwendeshamashataka mkuu kutaka kinga ya Rais Wulff iondolewe, chama kikuu cha upinzani cha Social Democrats, SPD, kiliunga mkono azma hiyo. Katibu Mkuu wa chama hicho Andrea Nahles amesema ni lazima Christian Wulff aondoke kwenye ofisi ya Rais.

''Tumekwishatamka wazi juu ya matukio haya kwamba lazima Rais Wulff ajiuzulu, na tumependekeza kwa Kansela Angela Merkel juu ya kumtafuta mtu mwingine wa kuchukua wadhifa wa Urais bila kujali anatoka chama gani cha kisiasa. Kwa sasa jambo hilo ni muhimu kulioko wakati wowote ule mwingine.'' Andrea Nahles alisema.

Chama cha Kijani na Chama cha mrengo wa kushoto vimetangaza misimamo inayofanana na huo wa SPD, kwamba bwana Wulff hana hadhi tena ya kuendelea kutumikia ofisi.

Kwa zaidi ya miezi miwili iliyopita, Rais Wulff amekabiliwa na shutuma kashfa nyingi, zikiwemo kupokea mkopo kutoka kwa mfanyabiashara tajiri, na kujaribu kunyamazisha vyombo vya habari visizungumzie kashfa zake. Hadi sasa alikuwa hajaonyesha nia ya kujiuzulu, na ingawa kufukuzwa madarakani ni jambo linalowezekana, kuna vizingiti vingi vya kisiasa kufanya hivyo.

Katika hali inayoashiria kuwa maji yamefika shingoni katika kashfa hii inayomhusu Rais Christian Wulff, Kansela Angela Merkel ameahirisha kwenye dakika ya mwisho asubuhi ya leo, safari yake kwenda Italia kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa nchi hiyo Mario Monti.

Mwandishi: Kinkartz/Daniel Gakuba/Reuters, dpa, AFP

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed