1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rajoelina aelekea Sychelles licha ya uasi wa kijeshi

Mohamed Dahman23 Julai 2012

Kiongozi wa Madagascar Andry Rajoelina ameelekea Sychelles kwa mazungumzo ya ana kwa ana na mpinzani wake mkuu aliyempinduwa madarakani Marc Ravalomanana licha ya uasi wa kijeshi uliotokea mwishoni mwa juma.

https://p.dw.com/p/15dOX
Rais Andry Rajoelina wa Madagascar.
Rais Andry Rajoelina wa Madagascar.Picha: AP

Wanajeshi walioasi waliitwaa kambi hiyo muhimu ilioko kilomita 10 kutoka katika mji mkuu wa Antananarivo wakati wa alfajiri ya Jumapili. Haifahamiki nini yalikuwa madai yao au manun'guniko yao, lakini kisa hicho kiligeuka kuwa kibaya baada ya kumpiga risasi na kumuuwa afisa wa kijeshi alietumwa kuzungumza nao.

Generali Raphael Ramasy, Mkuu wa majeshi ya Madagascar, ameiambia televisheni ya taifa, TVN, kwamba vurugu hizo zimedhibitiwa.

Ameongeza kusema kwamba koplo Kolo Mainty, kwa jina jengine Black, ameuwawa na wanajeshi wengine walioasi wamejisalimisha au kukamatwa.

Jeshi limesema Mainty, kiongozi wa uasi huo, alikuwa mlinzi wa zamani wa waziri wa zamani wa ulinzi.

Ramasy amesema raia wanne wamekamatwa, wanajeshi wawili walioasi na maafisa usalama wawili wamejeruhiwa.

Uasi haukuathiri mazungumzo

Kisiwa cha Madagascar kimekumbwa na machafuko ya kisiasa kwa miaka mitatu sasa tokea kongozi wa upinzani, Andy Rajoelina, kumpinduwa rais Marc Ravalomanana ambaye tokea wakati huo amekuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini.

Mwanajeshi wa kikosi maalum cha Madagascar.
Mwanajeshi wa kikosi maalum cha Madagascar.Picha: AP

Kwa mujibu wa msaidizi wa Ravalomanana, viongozi hao mahasimu walikuwa wamepangiwa kukutana wiki hii katika visiwa vya Sychelles, lakini mkutano huo haukutangazwa rasmi.

Jenerali mstaafu Phillipe Ramakavelo, ambaye ni mtaalamu wa siasa na mjumbe wa baraza la mpito, amesema uasi huo wa kijeshi unaweza kuwa na athari kwa mkutano huo.

Akiondoka kelekea Sychelles kwa ajili ya mkutano huo Rajoelina amewaambia waandishi wa habari waliokuwepo uwanja wa ndege kwamba Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imepunguza idadi ya wajumbe ili kwamba aweze kukutana ana kwa ana na Ravalomanana hapo Jumatano katika mkutano huo unaosimamiwa na jumuiya hiyo ya nchi wanachama 15.

Kwa upande wa uasi huo wa kijeshi,jeshi limesema kwamba kundi la wanajeshi wenye silaha lilivamia kambi iliko karibu na uwanja wa ndege wa nchi hiyo na kufyetuwa risasi hewani pamoja na kuzuwiya juhudi zozote zile za kuingia kwenye kambi hiyo.

Wanajeshi na wanamgambo waliizingira kambi hiyo na kutuma maafisa kuzungumza na wanajeshi walioasi. Limesema kwamba ilibidi iivamie kambi hiyo baada ya wanajeshi walioasi kumpiga risasi na kumuuwa mmojwapo wa wajumbe waliotumwa kuzungumza nao, Philibert Ratovoninna, mkuu wa huduma za mawasiliano jeshini.

Taarifa ya wizara ya ulinzi imesema uwanja wa ndege wa Ivato uko wazi. Wakati ubalozi wa Marekani nchini Madagascar ukisema safari za ndege za kuingia na kutoka katika uwanja huo zimefungwa, ubalozi wa Uingereza umesema uwanja wa ndege huo umefunguliwa tena na kwamba safari zingelianza leo hii.

SADC ni msuluhishi

Hapo mwezi wa Septemba vyama vikuu vya kisiasa kisiwani Madagascar vilisaini makubaliano chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo yalimthibitisha Rajoelina kuwa rais, kuruhusu kurudi nchini humo kwa Ravalomanana bila masharti, na kuandaa uchaguzi mkuu katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja.

Aliyekuwa rais wa Madagacsar, Marc Ravalomanana.
Aliyekuwa rais wa Madagacsar, Marc Ravalomanana.Picha: AP

Jumuiya ya SADC imewapa viongozi hao wawili mahasimu hadi tarehe 31 mwezi wa Julai kufikia makubaliano.

Mara kwa mara wanajeshi wamekuwa wakiingilia katika siasa za Madagascar tokea nchi hiyo ijipatie uhuru wake kutoka Ufaransa hapo mwaka 1960.

Sekta ya utalii ya kisiwa hicho imeathriwa vibaya kutokana na kukosekana utulivu wa kisiasa na kuwatia wasi wasi wafanya biashara wanaotaka kuwekeza katika sekta za mafuta, uchimbaji wa dhahabu na makaa ya mawe.

Mwandishi:Mohammed Dahman/RTR
Mhariri: Miraji Othman