1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rajoelina na Ravalomanana wa Madagascar wakutana

25 Julai 2012

Kiongozi wa Madagascar, Andry Rajoelina, amekutana na kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Marc Ravalomanana, katika visiwa vya Ushelisheli kufanya mazungmzo ya kumaliza tofauti zao.

https://p.dw.com/p/15eMc
Andry Rajoelina, kiongozi wa Madagascar
Andry Rajoelina, kiongozi wa MadagascarPicha: AP

Afisa mmoja wa serikali ya Ushelisheli amearifu kwamba mazungumzo baina ya kiongozi wa mpito wa Madagascar Rajoelina na mwenzake aliyemtangulia yalianza leo asubuhi katika kisiwa cha Desroches. Mazungumzo hayo yanahudhuriwa pia na rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye ni mpatanishi mkuu kati ya Rajoelina na Ravalomanana. Rais James Michel wa visiwa vya Ushelisheli pia amealikwa katika mazungumzo hayo yanayotarajiwa kumalizika leo jioni.

Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, yenye wanachama 15, imempa Rajoelina na mpinzani wake muda hadi tarehe 31 mwezi huu ili kumaliza tofauti zao. Kisiwa cha Madagascar kilichopo katika bahari ya Hindi kimekumbwa na migogoro ya kisiasa tangu mwezi Machi mwaka 2009, ambapo Rajoelina alimwondoa Ravalomanana madarakani kwa nguvu akisaidiwa na jeshi la nchi hiyo.

Mgogoro wa kisiasa waendelea tangu 2009

Rajoelina, ambaye kabla ya kuwa kiongozi wa nchi yake alikuwa anafanya kazi kama DJ, alikuwa na umri wa miaka 34 tu alipoingia madarakani, na hivyo ilibidi abadilishe katiba ya Madagascar ili aweze kugombea katika chaguzi zijazo. Hadi sasa kiongozi huyo ameshindwa kuungwa mkono na sehemu kubwa ya jumuiya ya kimataifa.

Watu waliomuunga mkono Rajoelina katika mapinduzi
Watu waliomuunga mkono Rajoelina katika mapinduziPicha: AP

Mwaka uliopita Rajoelina na Ravalomanana walisaini makubaliano ya kuandaa uchaguzi mkuu, lakini hadi sasa wameshindwa kutimiza makubaliano hayo kikamilifu. Pameshakuwa na mazungumzo baina ya viongozi hao wawili, lakini yalifanyika pamoja na wawakilishi wa vyama vyao. Wote wawili wamekuwa wakikwepa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana.

Jeshi la Madagascar, ambalo mara kwa mara hujiingiza katika siasa nchini humo, limechangia vikubwa kuinuka kwa Rajoelina, lakini mapinduzi ya mwaka 2009 yamesababisha taifa hilo kutengwa na Jumuiya ya Kimataifa, huku wafadhili wakiondoa misaada yao. Mataifa ya Afrika pia yameifutia Madagascar uwanachama katika jumuiya zake.

Ravalomanana atakiwa mahakamani

Kikwazo kikubwa kinachojitokeza katika mchakato wa kumaliza mgogoro wa kisiasa wa Madagascar ni kupatikana kwa masharti yatakayomruhusu Ravalomanana kurejea nchini mwake kutoka uhamishoni Afrika Kusini. Mwaka 2010, Ravalomanana, bila kuwepo mwenyewe mahakamani, alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa sababu ya kuuliwa kwa waandamanaji 30 mwaka 2009. Waandamanaji hao waliuliwa na kikosi maalum cha kumlinda rais.

Rais wa zamani wa Madagascar, Marc Ravalomanana
Rais wa zamani wa Madagascar, Marc RavalomananaPicha: AP

Tangu kukimbilia uhamishoni, rais huyo wa zamani ameshajaribu mara mbili kurejea Madagascar, lakini maafisa wa nchi hiyo kila wakati walimzuia yeye na mke wake kuingia. Ravalomanana anatakiwa kwenda kujibu mashtaka mbele ya mahakama moja ya Afrika Kusini ifikapo tarehe 1 Agosti mwaka huu. Wahanga wa machafuko yaliyotokea Februari 2009 wanataka awalipe fidia ya dola za kimarekani millioni 23

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp

Mhariri: Othman Miraji