1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RAMALLAH : Rice asema wakati umefika kwa taifa la Palestina

16 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7FW

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice amesema kwamba Rais George W. Bush anataka kulifanya suala kukomesha mzozo kati ya Israel na Wapalestina kuwa mojawapo ya vipau mbele vyake vya juu.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari na Rais Mahmoud Abbas wa Wapalestina mjini Ramallah Rice amesema mkutano wa kimataifa wa amani uliopangwa kufanyika nchini Marekani hapo mwezi wa Novemba lazima uwe makini na thabiti.

Rice amesema kwa kusema kweli wakati umefika wa kuanzishwa kwa taifa la Palestina na wakati umefika kwa Israel kuishi katika hali ya usalama ambayo itakuja kwa kuwepo kwa taifa jirani la amani na lenye demokrasia.Amesema wakati umefika kwa Wapalestina kuwa na taifa lao wenyewe.

Pande hizo mbili zinajaribu kuwa na waraka wa amani wa mwisho wa pamoja kabla ya mkutano huo wa mwezi wa Novemba.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amekuwa akishinikiza kuwepo kwa waraka usio na ufafanuzi wa kina wakati Wapalestina wanataka waraka wenye ufafanuzi ukiwa na ratiba kamili ya kuanzishwa kwa taifa la Palestina.