1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa atangaza vita dhidi ya rushwa

Bruce Amani
21 Desemba 2017

Kiongozi mpya wa chama tawala nchini Afrika Kusini African National Congress, ANC Cyril Ramaphosa na ambaye ana nafasi kubwa ya kuwa rais ajaye wa nchi hiyo, amesema kuwa ANC lazima ikomeshe rushwa ndani ya chama

https://p.dw.com/p/2pkG5
Südafrika ANC Parteitag Ramaphosa
Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Hadebe

Cyril Ramaphosa, ambaye wakati mmoja alipendelewa kumrithi Nelson Mandela, alitoa hotuba yake ya kwanza akiwa kiongozi wa chama wakati akikabiliwa na changamoto ya kuifufua mojawapo ya mataifa kubwa ya kiuchumi barani Afrika na imani ya umma katika chama cha ANC kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2019.

Hasira imeongezeka juu ya madai ya rushwa dhidi ya Rais Jacob Zuma, na baadhi ya wachambuzi walisema kuwa chaguo la mrithi Zuma kukiongoza ANC huenda likaligawanya vuguvugu hilo la ukombozi barani Afrika

Lakini Ramaphosa mwenye umri wa miaka 65, makamu wa rais wa Afrika kusini na mmoja wa wafanyabiashara matajiri kabisa nchini humo, alitangaza kuwa ni ushindi dhidi ya wanaotabiri mabaya.

Ramaphosa alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama katika kinyang'anyiro kikali dhidi ya Nkosazan Dlamini Zuma, ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Afrika na mke wa zamani wa Zuma. Atakuwa mgombea wa ANC katika uchaguzi wa 2019, ambapo anatarajiwa kushinda. Baadhi ya wachambuzi wanaonya kuwa kama chama kitaendelea kupoteza uungwaji mkono huenda kikalazimika kuunda serikali ya muungano kwa mara ya kwanza.

Südafrika ANC Parteitag Nkosazana Dlamini-Zuma
Nkosazana Dlamini Zuma aligombea uongozi wa chamaPicha: picture-alliance/AP Photo/T. Hadebe

Wakosoaji ndani na nje ya chama wanamtolea wito Ramaphosa kumtolea wito Zuma kujiuzulu wadhifa wa urais ili kuimarisha nafasi za ANC kushinda uchaguzi wa 2019.

ANC ambayo ilichukua madaraka mwaka wa 1994 katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini Afrika, kilikuwa na matokeo mabaya kabisa katika uchaguzi wa mwaka jana wakati kilipoteza viti katika miji mikubwa ukiwemo wa kibiashara Johannesburg na mji mkuu Pretoria. Badala yake, Ramaphosa alimshukuru Zuma katika hotuba yake kwa uongozi wake wa muongo mmoja ambao ulihakikisha kuwa mpango wa Afrika Kusini wa kutoa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi ulifanikiwa kuwa mkubwa kabisa duniani.

Lakini Ramaphosa pia alitoa ombi la kuwapo na "uongozi wa uwajibikaji” baada ya hasira ya umma kuhusiana na madai ya ushawishi wa Zuma na wengine wa maslahi binafsi ya kibiashara.

Ushindi mwembamba wa Ramaphosa wa chini ya kura 200, na ukweli kwamba nusu ya uongozi mkuu wa ANC sasa unajumuisha washirika wakubwa wa Zuma, huenda ukafanya mambo kuwa magumu katika kutimiza ahadi zake za kukiunganisha chama hicho kilichogawika pakubwa na kuleta mageuzi katzika uchumi na utawala wa Afrika Kusini.

Kiongozi huyo mpya wa ANC alisema chama hicho kitaendelea kuangazia mbinu za kuondoa umaskini na ukosefu wa ajira ambao kiwango chake kinakaribia asilimia 30, na kuitekeleza sera yake ya "kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi” yanayolenga upunguza ukosefu wa usawa uliowekwa chini ya enzi ya ubaguzi wa rangi.

Megeuzi ya ardhi ni uamuzi wa kwanza muhimu uliofikiwa na viongozi wapya wa chama hicho. Kwamba urithi wa mashamba bila fidia unapaswa kuwa miongoni mwa taratibu zinazoweza kutumiwa na serikali katika kutimiza mageuzi ya ardhi na ugawaji upya.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo