1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rangoon. Utawala wa kijeshi waweka amri ya kutotembea usiku.

29 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBLn

Hatua ya marufuku ya kutotembea usiku imeanza kufanya kazi mjini Rangoon baada ya siku ya tatu ya msako uliofanywa na utawala wa kijeshi wa Burma. Hapo mapema , makundi ya watu yaliwakejeli polisi , wakati wanajeshi walipambana na mamia kadha ya waandamanaji. Risasi na mabomu ya gesi ya kutoa machozi vilifyatuliwa hewani dhidi ya makundi hayo ya waandamanaji. Taarifa za mtandao wa Internet kutoka nchini humo zimekatwa.

Vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo vimesema kuwa idadi ya watu waliouwawa siku ya Alhamis ni tisa, lakini wanadiplomasia wa kimataifa wamesema kuwa idadi hiyo inawezekana kuwa juu zaidi. Ripoti ambazo hazikuthibitishwa zimesema kuwa baadhi ya wanajeshi walibadilishwa baada ya kukataa amri ya kuwafyatulia risasi watawa. Japan imesema kuwa inatuma mjumbe ambaye atachunguza kuuwawa kwa mwandishi habari mpiga picha kutoka nchi hiyo siku ya Alhamis.

Utawala wa Marekani jana Ijumaa uliweka vikwazo vya visa kwa zaidi ya wawakilishi 30 wa utawala wa kijeshi wa Myanmar pamoja na familia zao.

Mwakilishi maalum wa umoja wa mataifa Ibrahim Gambari yuko njiani hivi sasa kwenda nchini Burma akitokea Singapore ili kusaidia katika mazungumzo baina ya utawala wa kijeshi na wapinzani wake wanaodai demokrasia.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice amesisitiza kuwa utawala huo wa Mynamar unapaswa kumpa mjumbe maalum wa umoja wa mataifa ushirikiano katika ziara yake huko.

Kutokana na kile kinachotokea katika mitaa ya Rangoon , nilikuwa na matumaini kuwa baraza la usalama la umoja wa mataifa lingechukua hatua kali zaidi. Lakini tunaridhika kwa kuwa balozi Ibrahim Gambari anakwenda huko kwa niaba ya katibu mkuu ambapo pia tulikuwa na majadiliano wakati wa uzinduzi wa ziara hiyo kuwa atapeleka ujumbe kuwa sisi tuna msimamo wa pamoja katika kusisitiza kwamba wampokee na wamsaidie katika maombi yake yote.