1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rasimu ya mabadiliko ya tabia nchi yaidhinishwa

14 Desemba 2014

Takriban nchi 190 zimekubaliana Jumapili (14.12.2104) kuidhinisha rasimu ya vipengee muhimu kuelekea makubaliano ya dunia ya mwaka 2015 yanayotazamiwa kufikiwa Paris kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/1E42Q
Katibu Mtendaji wa Kamati ya Mabadiliko ya tabia nchi ya Umoja wa Mataifa Christiana Figueres na Mwenyekiti wa mkutano na waziri wa mazingira wa Peru Manuel Pulgar wakishangilia kuidhinishwa kwa makubaliano mjini Lima. (14.12.2014)
Katibu Mtendaji wa Kamati ya Mabadiliko ya tabia nchi ya Umoja wa Mataifa Christiana Figueres na Mwenyekiti wa mkutano na waziri wa mazingira wa Peru Manuel Pulgar wakishangilia kuidhinishwa kwa makubaliano mjini Lima. (14.12.2014)Picha: AFP/Getty Images/C. Bouroncle

Chini ya makubaliano hayo yaliofikiwa katika mji mkuu wa Peru Lima yaliopewa jina " Wito wa Lima wa Hatua ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi ",serikali zinatakiwa ziwasilishe mipango ya taifa ya kudhibiti utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira kufikia tarehe 31 Machi mwaka 2015 tarehe ya mwisho isio rasmi ili kuunda msingi wa makubaliano ya dunia yaliopangwa kufikiwa katika mkutano wa kilele wa mazingira mjini Paris mwakani.

Takriban maamuzi yote magumu juu ya namna ya kupunguza mabadiliko ya tabia nchi yameahirishwa hadi utapofika wakati huo. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema kuna mengi yanayohitajika kufanyika huko Paris mwakani.

Rasimu ya maandishi ya makubaliano hayo yaliofikiwa katika siku mbili za muda wa ziada baada ya mazungumzo hayo ya wiki mbili kukaribia kusambaratika yamezituliza nchi zinazoinukia kiuchumi zikiongozwa na China na India ambazo zilikuwa na wasi wasi kwamba rasimu za awali zilizitwisha mzigo mkubwa zaidi nchi zinazoinukia kiuchumi kwa kulinganisha na nchi tajiri.

Waziri wa mazingira wa India Prakash Javedekar amekaririwa akisema tumepata kile tulichokitaka akimaanisha rasimu hiyo imehifadhi hoja iliotajwa katika makubaliano ya mazingira ya mwaka 1992 kwamba nchi tajiri inabidi ziongoze njia katika kupunguza utowaji wa gesi chafu zenye kuathiri mazingira.

Nchi tajirí zaridhika

Pia rasimu ya makubaliano hayo imeziridhisha nchi tajiri zikiongozwa na Marekani ambazo zimesema wakati umefika nchi zenye uchumi unaokuwa kwa haraka sana kudhibiti utowaji wa gesi hizo unaongezeka kwa haraka sana.China hivi sasa ndio mtowaji mkubwa kabisa wa gesi zenye kuathiri mazingira ikifuatia na Marekani,Umoja wa Ulaya na India.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Mabadiliko ya Tabia Nchi na Nishati Mguel Arias Canete katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi Lima.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Mabadiliko ya Tabia Nchi na Nishati Mguel Arias Canete katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi Lima.Picha: AFP/Getty Images/C. Bouroncle

Mjumbe maalum wa Marekani katika suala la Mabadiliko ya Tabia nchi Todd Stern amesema makubalino ya pamoja kati ya Marekani na China yaliofikiwa mwezi uliopita kudhibiti utowaji wa gesi chafu yamesaidia kuonyesha njia za kupunguza mzozo kati ya nchi tajiri na maskini.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Mabadiliko ya Tabia Nchi na Nishati Mguel Arias Canete ameliambia shirika la habari la Uingereza mwishoni mwa mazungumzo hayo ya kupunguza mafuriko, kuenea kwa jangwa, kuongezeka kwa kiwango cha joto na kupanda kwa kina cha bahari kwamba huo ulikuwa ni waraka mzuri kuwaelekeza Paris.

Makubaliano ni dhaifu mno

Hata hivyo baadhi ya makundi ya watetezi wa mazingira yamesema makubaliano hayo yaliofikiwa Lima ni dhaifu mno.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon (katikati) akiwa katiika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi Lima.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon (katikati) akiwa katiika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi Lima.Picha: picture-alliance/landov

Samantha Smith wa shirika la Mfuko wa Kuhifadhi Wanyama Pori WWF akizungumzia mfululizo wa rasimu za Lima amesema wametoka kwenye rasimu dhaifu na kuingia dhaifu zaidi hadi kuwa dhaifu kabisa.

Wazo la makubaliano hayo ya Umoja wa Mataifa la majukumu kutimizwa na mataifa yote tafauti na Itifaki ya Kyoto ambapo nchi tajiri tu zililazimika kupunguza utowaji wa gesi chafu.

Mtindo mpya

Christiane Figueres mkuu wa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi wa Umoja wa Mataifa amesema imegunduwa njia mpya kufafanuwa majukumu ya nchi tajiri na maskini na kwamba huo ulikuwa ni ufumbuzi muhimu sana.

Katibu Mtendaji wa Kamati ya Mabadiliko ya tabia nchi ya Umoja wa Mataifa Christiana Figueres.
Katibu Mtendaji wa Kamati ya Mabadiliko ya tabia nchi ya Umoja wa Mataifa Christiana Figueres.Picha: AFP/Getty Images/E. Benavides

Jennifer Morgan wa jopo la ushauri la Taasisi ya Rasilmali za Dunia amesema kile wanachokiona na aina mpya ya ushirikiano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ambapo nchi zote zinashiriki huku kukiwa na kanuni mpya.

Kwa mujibu wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya mabadiliko ya tabia nchi ahadi zilizochanganywa na kutolewa na mataifa yote yumkini ikawa ni dhaifu mno kuweza kufanikishwa huko Paris lengo la kupunguza ongezeko la ujoto lililoafikiwa la digrii mbili za nyuzi joto ambacho ni kiwango kilioko juu ya enzi ya kabla ya viwanda.

Chini ya makubaliano hayo ya Lima ahadi za taifa zitaongezwa kwenye repoti inayotakiwa iwasilishwe kufikia Novemba Mosi mwaka 2015 kutathmini taathira za kujumuishwa kwao kwa pamoja katika kupunguza ongezeko la ujoto.

Mhariri : Mohamed Dahmam /Reuters/AFP/AP

Mhariri : Amina Abubakar