1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ratiba ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010

5 Desemba 2009

-

https://p.dw.com/p/Kqlq
Rais wa shirikisho la Soka la Italia, Giancarlo Abete,akimkabidhi kombe rais wa FIFA Joseph Blatter ikishuhudiwa na rais wa Africa Kusini Jacob Zuma wakati wa sherehe za DrooPicha: picture alliance / dpa

Haiwi Haiwi hatimaye imekuwa, Mashabiki wa soka kote ulimwenguni sasa wanajua, timu zao zitapambana na timu zipi, katika kidumbwedumbwe cha kombe la dunia, mwakani nchini Afrika Kusini. Katika hafla iliyonoga mjini Cape Town, kura ilipigwa kuzipanga katika makundi timu 32 zitakazoshiriki katika kombe la dunia. Kuna makundi manane, na kila kundi lina timu nne. Afrika inawakilishwa na timu sita, je zipo katika makundi gani, rahisi au magumu?

Michuano ya kombe la dunia itaanza tarehe 11 juni hadi 11 juli mwakani na kuna makundi manane ambayo ni A hadi H. Na hivi ndivyo ratiba ya michuano hiyo ya kombe la dunia itakavyokuwa baada ya droo ya hapo jana.Wenyeji Afrika Kusini wako katika kundi A watajitupa uwanjani Ijumaa ya tarehe 11 Juni kuminyana na Mexico katika uwanja wa Johannesberg wa Soccer City saa 16.00 jioni ambapo pia katika kundi hilo wamo Uruguay watakaocheza na Ufaransa mjini Cape Town. Kundi B katika mechi itakayochezwa jumamosi Korea Kusini itapambana na Ugiriki huku Argentina nayo ikipangiwa kucheza na Nigeria .Nchi washirika katika jukwaa la siasa za kimataifa, Uingereza na Marekani zitapigana kikumbo katika kundi C jumamosi ya mwezi juni tarehe 12. Katika kundi la C pia zitakutana uwanjani huko Polokwane,timu ya Algeria na Slovenia.

WM-Auslosung Kapstadt Süafrika Fußball Weltmeisterschaft
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela akihutubia taifa kwa njia ya Video mwanzoni mwa sherehe za droo ya michuano ya kombe la dunia mwaka 2010Picha: AP

Timu nyingine ya Afrika ambayo inategemewa na mashabiki wake kufanya vizuri ni Ghana nayo imeangukia katika kundi la D ikipangiwa kuonyeshana nguvu na Serbia mjini Pretoria.

Ujerumani ambao ni wenyeji wa kombe la dunia lililopita wako katika nafasi nzuri ya kuonyesha misuli yao katika kundi hilo la D wakikutana na Australia mjii Durban hiyo itakuwa ni juni 13.

Na katika kundi E Uholanzi watapambana na Denmark huku Cameroon ikipangiwa kucheza na Japan. Katika kundi F zimepangwa Italy kucheza na Paraguay na Newzealand ikiwa na Slovakia. Ivory Coast itakabiliana na Ureno katika mechi ya kufa kupona huko Port Elizabeth hilo likiwa ni kundi la G ambapo pia kuna mchuano kati ya Brazil na Korea Kaskazini. Kundi la mwisho la H litawakutanisha Honduras na Chile na pia Spain itakayochuana na Uswisi mjini Durban.

Hivyo ndivyo timu zilivyopangwa na bila shaka wako waliofurahia mpangilio huo na walioungulika.Wenyeji Afrika kusini wamesema wanaimani kwamba wataipiga kikumbo Mexico katika mchuano wa duru ya kwanza. Bila shaka timu hiyo ya Afrika kusini ni mojawapo kati ya Timu za Afrika zitakazokuwa na kibarua kigumu hasa ikizingatiwa kwamba itapambana na mabingwa wa zamani wa kombe hilo la dunia Uruguay na Ufaransa katika kundi hilo la A.Kocha wa Uingereza Fabio Capello pia amefurahishwa sana na droo hiyo lakini pia amesema hatarajii mechi hizo kuwa rahisi.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/RTRE

Mhariri:P.Martin