1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raundi ya pili ya uchaguzi kufanyika Februari 3 nchini Serbia

Josephat Charo21 Januari 2008

Rais Borisf Tadic kupambana na mpinzani wake mkuu Tomislav Nikolic

https://p.dw.com/p/CvZa
Rais Boris Tadic (kushoto) na Tomislav NikolicPicha: picture-alliance/ dpa

Kiongozi wa upinzani mwenye msimamo mkali nchini Serbia, Tomislav Nikolic, ameshinda awamu ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini humo kufuatia uchaguzi uliofanyika hapo jana. Hata hivyo kiongozi huyo analazimika kushindana tena na mpinzani wake mkuu, rais wa Serbia, Boris Tadic, katika awamu ya pili ya uchaguzi. uliopangwa kufanyika mwezi ujao.

Mahasimu wawili wa kisiasa nchini Serbia wameanza kampeni mpya hii leo baada ya awamu ya kwanza ya uchaguzi. Rais anayepigania mageuzi wa Serbia, Boris Tadic, na mpinzani wake mwenye msimamo mkali, Tomislav Nikolic, wameanza juhudi mpya za kutafuta kura baada ya uchaguzi wa mwishoni mwa juma kuwalazimu washindane tena katika awamu ya pili ya uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 3 mwezi ujao wa Februari.

Akizungumza baada ya kushinda awamu ya kwanza ya uchaguzi dhidi ya rais Tadic, kwa kupata asilimia 40 ya kura, Tomislav Nikolic amesema

´Serbia imedhihirisha kwamba imelielewa ombi langu. Hatujawahi kuukaribia ushindi namna hii. Hakuna anayeweza kutuzuia. Na kila anayetaka kuiunganisha Serbia, maana Serbia ni nchi moja, hapaswi kuzuiliwa.´

Rais Tadic amefanya kampeni katika mkoa wa kaskazini wa Vojvodina, ulio na wakaazi milioni mbili wa makabila mbalimbali

kutoka nchi zaidi ya 20, wakiwezo raia laki tatu wa Hungary. Rais Tadic ana matumaini ya kuwavutia asilimia 2.2 ya wapigaji kura waliowapigia kura wagombea urais walioshindwa dhidi ya mpinzani wake mwenye nasaba ya Hungary. Viongozi wote wawili wanapinga uhuru kamili wa jimbo la Kosovo kutoka kwa Serbia.

Kiongozi wa upinzani Tomislav Nikolic, alitarajiwa hii leo kuuhutubia umma na kuzindua mipango yake mipya ya kampeni kwa ajili ya awamu ya pili ya uchaguzi wa mwezi ujao, dhidi ya mpinzani wake rais Tadic.

Wagombea wote wawili wanatarajiwa kuwalenga wapigaji kura waliowaunga mkono wagombea wa urais walioshindwa katika uchaguzi wa jana, hususan wafuasi wa waziri wa miundombinu Velimir Ilic aliyeshika nafasi ya tatu katika matokeo ya uchaguzi wa jana, Cedomir Jovanovic, aliyeshinda asilimia 5.9 ya kura na msoshalisti, Mrkonjic, aliyepata asilimia sita.

Rais Boris Tadic amewataka wapigaji kura wote waonyeshe kwamba Serbia haitaachana na mkondo wake kuelekea Ulaya ulioanza kuchukuliwa tangu kuanguka madarakani kwa rais wa zamani hayati Slobodan Milosevic mnamo mwaka wa 2000.

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya uchaguzi wa jana rais Tadic amesema ana hakika Waserbia wataaamua kuunga mkono juhudi za Serbia kuwa na uhusiano wa karibu na Ulaya.

´Sitaruhusu hali ya kutoridhika na wasiwasi viwe na nafasi kwa mara nyingine tena nchini Serbia lakini nitatoa ujumbe dhidi ya machafuko. Sitaruhusu Serbia irudi nyuma katika miaka ya 90. Tutaendelea na kuipigania Kosovo ili kuendeleza dhima ya nchi yetu lakini pia hatutaachana na juhudi zetu za kuegemea Ulaya katika siku za usoni.´

Tume ya uchaguzi nchini Serbia ilitarajiwa kutoa matokeo rasmi ya mwisho ya uchaguzi wa jana hii leo. Lakini hata hivyo matokeo hayo hayatarajiwi kusababisha mabadiliko makubwa ya matokeo yaliyotolewa kufikia hivi sasa.

Wachambuzi wanasema idadi kubwa ya Waserbia walijitokeza katika uchaguzi huo inadhihirisha vipi walivyoupa umuhimu mkubwa uchaguzi huo. Idadi ya wapigaji kura katika raudniya pili ya uchaguzi inatarajiwa kuongezeka.