1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RB Leipzig yakataa kusalimu amri

Sekione Kitojo
2 Novemba 2016

Timu tatu hadi sasa hazijaonja kipigo katika Bundesliga. Bayern Munich, RB Leipzig na TSG Hoffenheim zimeendelea kufanya vizuri  katika msimu huu na zinaonekana kufanya mabadiliko ya haraka kwa wachezaji

https://p.dw.com/p/2S1Cl
Bundesliga | SV Darmstadt 98 vs RB Leipzig | 9 Spieltag 2016/2017
Picha: Getty Images/Bongarts/A. Scheuber

Kwa  upande  wa  mabingwa   Bayern  Munich hali  hiyo  ilitarajiwa. Kwa  upande  wa  Leipzig  ambayo imepanda  daraja  msimu  huu  na  Hoffenheim  ambayo  ni timu  ya  kijijini  hilo  halikutarajiwa. Kwa  upande  wa Hoffenheim  mafanikio  yanaweza  kuwekwa  mabegani mwa  kocha  kijana  kabisa  katika  Bundesliga , Julian Nagelsmann, akiwa  na  umri  wa  miaka  29. Kikosi  chake kilionesha  ukomavu  mkubwa  katika  mpambano  dhidi  ya Hertha  BSC  Berlin  na  kupata  ushindi  wa  bao 1-0 lililofungwa  na  mlinzi  wa  kati  Niklas Suele ambaye anasema  alitamani  sana  kufunga  bao  kwa  muda  mrefu na  sasa  ametimiza  ndoto  yake.  Huyu  hapa  Sule.

Nilitamani  sana  kufunga  bao. Ilichukua  muda. Kwa  hiyo ni  bao  muhimu  sana  kwangu  na  lilikuwa  muhimu  sana kwa  timu  yetu. Tumefanikiwa  leo  kwa  kuonesha  mchezo mzuri  sana. Wote  tumefurahi, kwamba  tumeweza  kupata hapa  nyumbani  pointi  tatu. Hilo  lilikuwa  muhimu  sana.

Mshambuliaji wa Cologne Anthony Modeste amekuwa moto wa kuotea mbali
Mshambuliaji wa Cologne Anthony Modeste amekuwa moto wa kuotea mbaliPicha: picture-alliance/dpa/M. Becker

FC Kolon ilipata  ushindi  wa  mabao  3-0  jana  Jumapili , na  inaendelea  kubaki  juu  katika  msimamo  wa  ligi. Mshambuliaji wa Kolon  Antony Modeste  alipachika  mabao yote  matatu  jioni  ya  jana  na  kuongoza  orodha  ya mafungaji  mabao  katika  Bundesliga  akiwa  na  mabao 11  katika  michezo  9, akifuatiwa  nyuma  na  Robert Lewandowski  wa  bayern  Munich  na  Pierre  Emerick Aubamiyang  wa  Borussia  Dortmund. Mchezaji  wa  FC Kolon  Simon Zoller  anasema. "Nafikiri , kwamba  msimu  huu  tuna  kila  fursa  ya kushangilia. Nafikiri  leo, kwa  msingi  wa  kipindi  cha  pili , tumestahili  matokeo  hayo. Kwa  kuwa  Hamburg  walikuwa na  wachezaji  pungufu  uwanjani  tulitumia  vizuri  fursa hiyo  na  kupata  mabao  matatu, ambapo  mwishoni  ni ushindi tuliostahili pia.

RB Lepzig sio  tu  haijafungwa  msimu  huu , lakini  pia inashangaza  kila  mtu  kwa  kuwa  timu  inayoifuata Bayern  Munich  katika  nafasi  ya  pili. Timu  hiyo iliyopanda  daraja  msimu huu  ilishinda  kwa  mabao  2-0 dhidi  ya  Darmstadt  siku  ya  Jumamosi. Wageni  hao katika  Bundesliga  tayari  imejikusanyia   pointi 21  na inabakia  katika  nafasi  ya  juu   karibu  na  Bayern  Munich ambayo  ina  pointi  23. Tulikuwa  na  kibarua  kigumu sana  ambacho  tulikitekeleza  kwa  ustadi  mkubwa  sana, amesema  kocha  wa  Leipzig Ralph Hasenhuttl. Mshambuliaji  wa  Leipzig  Timo  Werner  alikuwa  na  haya ya  kusema. "Tulistahili !  nafikiri , katika  sehemu  ya  kipindi  cha kwanza  tulionesha  wazi. Pengine  hatukuweza  kupata fursa  ya  kulazimisha  kupata  bao, lakini  tulitawala. Naamini  katika  kipindi  cha  kwanza  tulipata  bao  la kuongoza, kwa  kuwa  tulifunga  bao  , na  halikuwa  la kuotea. Na  ndio  sababu  hata  mwisho  wa  mchezo  kwa ushindi  huu  tulistahili. Bayern Munich  haikufanya  makosa  na  kuibamiza  tena Augsburg  kwa  mabao  3-1. Katikati  ya  wiki  timu  hizo zilikutana  katika  kombe  la  shirikisho  DFB Pokal  na Bayern  ilishinda  kwa  idadi  hiyo  hiyo  ya  mabao.

Schalke na BVB walikabana koo na bila kupatikana mshindi
Schalke na BVB walikabana koo na bila kupatikana mshindiPicha: Getty Images/AFP/P. Stollarz

Katika  pambano  la  watani  wa jadi  Borussia  Dortmund na  Schalke 04  hakuna  mbabe.  Mchezo  huo  uliochezwa katika  uwanja  wa  Signal Iduna Park  uliishia  sare  ya  bila kufungana. Mlinzi  wa  Schalke 04  Benedikt  Howedes kuhusu  pambano  hilo  la  watani  wa  jadi  anasema. "Tunaridhika  na  matokeo  ya  mchezo  huo. Katika  kipindi cha  kwanza , nadhani  , tulifanya  vizuri. Tulipata  fursa nzuri  zaidi  za  kufunga  bao. Katika  kipindi  cha  pili Dortmund ilikuja  juu, na  nafikiri  katika  vipindi  vyote kwa kiasi  fulani  tulifanya  vizuri."

Leverkusen  ilipata  ushindi  dhidi  ya  VFL  Wolfsburg , na Freiburg  ikapata  ushindi  wake  wa  kwanza  ugenini  dhidi ya  SV Werder  Bremen. Vipigo  hivyo  kwa  Werder Bremen  na  hasa  Wolfsburg vimeibua  mjadala  mpya  wa makocha  wa  timu  hizo. Wolfsburg  ilimtimua  kocha  wake wa   muda  mrefu  Dieter  Hecking  na  kumpa  kazi  hiyo kocha  wa  timu  ya  vijana  wa  timu  hiyo Valerien Ismail ambaye  hajaipatia  timu  hiyo  uwezo  wa  kushinda , ikiwa imepata  ushindi  mara  moja  tu  na  kufungwa  mara tano na  sare tatu. Bado  Wolfsburg  inaendelea  kusaka  kocha atakayeipatia  timu  hiyo  uwezo  wa ke  tena  wa  kushinda. Kuna  tetesi  kwamba  Wolfsburg  imeanza  mazungumzo na  kocha  Andre Villas Boas  ili  kuinoa  timu  hiyo. Bremen hali  kadhalika  bado  inasubuka  kutoka  katika  janga  la kupoteza  michezo  ikiwa  imepoteza  michezo 6, sare  moja na  ushindi  mara  mbili.

Low arefusha mkataba wake na timu ya Ujerumani

Wakati  huo  huo  kocha  Joachim Loew  aliyeiletea Ujerumani  kombe  la  dunia  amerefusha  mkataba  wake na  shirikisho  la  kandanda  nchini  Ujerumani  DFB. Loew mwenye  umri  wa  miaka  56 , ambaye  amekuwa  kocha wa  timu  ya  taifa  Die Mannschaft , tangu  mwaka  2006 na  kupata  ushindi  wa  kombe  la  dunia  mwaka  2014, amesema  majadiliano  kuhusiana  na  mkataba  mpya  na shirikisho  hilo  yamekwenda  vizuri  na  hakukuwa  na sababu  ya  kutorefusha  mkataba  huo.Rais  wa  shirikisho hilo  alisifu  kazi  ya  Loew  katika  timu  ya  taifa na kusema  ni  kocha  bora  kabisa  ambae tunaweza kumfikiria.Loew ambaye  mkataba  wake  ulikuwa  unaishia mwaka  2018  katika  kombe  la  dunia nchini  Urusi, ataendelea  kufanyakazi  na  benchi lake  la  ufundi  hadi mwaka  2020.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf saumu