1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Real, Barca zafungua mwaka 2015 kwa kipigo

5 Januari 2015

Baada ya kumaliza mwaka 2014 kwa mafanikio makubwa, Real Madrid imeufungua mwaka mpya wa 2015 kwa kipigo cha kwanza tangu mwezi Septemba.

https://p.dw.com/p/1EFEY
FC Valencia Real Madrid 2:1 4.1.2014
Picha: Jose Jordan//AFP/Getty Images

Madrid iliteleza kwa kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Valencia na kufikisha mwisho mlolongo wa ushindi wa michezo 22 katika mashindano yote. Hata hivyo , Barcelona imeshindwa kutumia fursa hiyo ya kuteleza kwa Real Madrid baada ya nayo kuonja " joto ya jiwe" na kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Real Sociedad na kuendelea kubaki nyuma ya Real inayoongoza ligi hiyo ya Uhispania , La Liga.

David Moyes Porträt
Timu yake David Moyes, ya Real Sociedad iliifanikiwa kuwadhibiti washambuliaji mahiri wa BarcelonaPicha: Reuters

Real Madrid haijapoteza mchezo ama kutoka sare katika mashindano yote inayoshiriki tangu pale ilipozabwa mabao 2-1 na Atletico Madrid Septemba 13, na kuweza rekodi nchini Uhispania kwa ushindi mfululizo.

Barcelona ilikuwa na nafasi ya kuweza kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi ikiipita Real , lakini ilipoteza mchezo wake dhidi ya Real Sociedad kufuatia bao la kujifunga mwenyewe lililotiwa wavuni na mlinzi Jordi Elba katika dakika ya pili. Washambuliaji nyota Lionel Messi na Neymar waliingia uwanjani kama wachezaji wa akiba katika kipindi cha pili, lakini walishindwa kuokoa jahazi hilo lililokwisha zama.

Rayo Vallecano pia ilitokea nyuma na kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Getafe. Eibar, wakati huo huo , imeendelea kufanya vizuri baada ya kurejea katika ligi ya daraja la kwanza msimu huu kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Espanyol na kusogea hadi katika nafasi ya nane ya msimamo wa ligi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre , afpe , dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga