1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Real Madrid yaiduwaza Borussia Dortmund

3 Aprili 2014

Real Madrid imeuweka mguu mmoja katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa mara ya nne mfululizo baada ya kuizaba Borussia Dortmund mabao matatu kwa bila uwanjani Santiago Bernabeu

https://p.dw.com/p/1BaUP
UEFA Champions League Real Madrid Borussia Dortmund
Picha: picture-alliance/dpa

Huku wakilenga kulipiza kisasi kichapo cha msimu uliopita mikononi mwa Wajerumani hao, Madrid walianza mechi ya jana kwa kasi, na wakapata goli la kwanza katika dakika ya tatu wakati Gareth Bale alipotikisa wavu wa BVB kutokana na pasi ya Dani Carvajal.

Isco alifanya mambo kuwa mawili kwa bila katika dakika ya 27 kabla ya Cristiano Ronaldo kufunga goli lake la 14 la Ligi ya Mabingwa msimu huu na kuifikia rekodi ya mabao iliyowekwa na Lionel Messi miaka miwili iliyopita. Hata hivyo mshambuliaji huyo nyota alilazimika kuchechemea na kuondoka uwanjani kutokana na kile kilichoonekana kuwa ni jeraha dogo lagoti ambalo baadaye kocha Carlo Ancelotti alisema siyo kitisho kikubwa.

Hata hivyo Real wanastahili kwenda Ujerumani kwa mkondo wa pili wakiwa na kumbukumbu za kichapo cha magoli manne kwa moja walichopata mikononi mwa vijana wa Jurgen Klopp katika nusu fainali msimu uliopita. Klopp aliwalaumu vijana wake kwa kupoteza kutumia nafasi zao, na pia kwa kutokuwa imara uwanjani na ndio maana wakafungwa magoli ya rahisi. Dortmund walianza kipindi cha pili kwa kasi na Pierre-Emerick Aubameyang ambaye alitwikwa mzigo mkubwa wa pengo lililoachwa na Robert Lewandowski katika safu ya mashambulizi lakini akapoteza nafasi kadhaa. Henrikh Mkhitaryan kisha akapoteza nafasi nyingine baada ya shuti lake kwenda nje baada ya kumgonga beki wa Real Pepe.

Cristiano Ronaldo amefikisha magoli 14 katika dimba la mwaka huu, na kuifikia rekodi ya Lionel Messi
Cristiano Ronaldo amefikisha magoli 14 katika dimba la mwaka huu, na kuifikia rekodi ya Lionel MessiPicha: Getty Images

Chelsea yazidiwa nguvu Paris

Katika mechi nyingine goli la kibinafsi lake Javier Pastore katikadakikaya mwisho liliwapa ushindi wenyeji Paris Saint-Germain wa magoli matatu kwa moja dhidi ya Chelsea. Goli la mapema lake Ezequiel Lavezzi na bao la kujifunga lake David Luiz na penalty iliyofungwa na Eden Hazard baada ya beki wa PSG Thiago Mota kumwangusha Oscar kwenye kijisanduku, lilionekana kuwapa PSG faida ndogo ya kupeleka katika mchuwano wa marudiano Uingereza. Lakini sasa goli la Pastore limewapa fursa kubwa mabingwa hao wa Ufaransa kuingia katika nusu fainali. Mshambuliaji nyota wa PSG Zlatan Ibrahimovic alichechemea na kuondolewa uwanjani katika kipindi cha pili kutokana na jeraha ambalo huenda likamweka nje ya mkondo wa pili.

Kocha wa Chelsea Jose Mourinho aliwalaumu wachezaji wake akisema walikuwa taabani baada ya kushindwa kuzitumia vyema nafasi chache walizopata. Na hasa goli la tatu, Mourinho aliwashutumu vikali mabeki wake akiilitaja kuwa bao la kijinga ambalo timu kama Chelsea haifai kufungwa. Amesema bado watajaribu kufanya wawezalo katika mechi ya marudiano. Kocha wa PSG Laurent Blanc hata hivyo amesema bado kibarua hakijaisha, kwa sababu Chelsea wana uwezo wa kujikomboa na kufanya mambo kuwa magumu katika uwanja wao wa nyumbani wiki ijayo.

Mwandishi. Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu