1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rias Bush amuunga mkono Wolfowitz

Josephat Charo13 Aprili 2007

Rais George W Bush wa Marekani amesema abado anamuung amkono rais wa benki ya dunia, Paul Wolfowitz, licha ya kashfa inayomkabili inayohusu kuongezwa mshahara mkubwa mpenzi wake Shah Riza uliozusha manung´uniko miongoni mwa wafanyakazi wa benki ya dunia.

https://p.dw.com/p/CB4j
Rais wa benki ya dunia Paul Wolfowitz
Rais wa benki ya dunia Paul WolfowitzPicha: AP

Rais George W Bush wa Marekani amesema hii leo kwamba bado anamuunga mkono rais wa benki ya dunia, Paul Wolfowitz, licha ya kashfa ya upendeleo aliouoyesha kwa mpenzi wake mzaliwa wa Libya, Shaha Riza. Msemaji wa Ikulu ya white house mjini Washington, Dana Perino, amesema rais Bush ana imani na bwana Wolfowitz na kazi anayoifanya katika benki ya dunia.

Huku miito ikizidi kumtaka Paul Wolfowitz ajiuzulu, wakurugenzi watendaji wa bodi ya benki ya dunia wametoa taarifa ambayo imemuweka mahali pabaya kiongozi huyo. Bodi hiyo imaehirisha mkutano wake wa leo kuzungumzia swala hilo lakini ikasema itafanya haraka kuamua itakavyoishughulikia kashfa hiyo.

Baada ya mkutano wa dharura jana ulioendelea mpaka usiku, bodi hiyo ilitoa maelezo ya kina kuhusu matokeo ya uchunguzi wao kuhusiana na mzozo unaomhusu Wolfowitz na mpenzi wake Shaha Riza. Kurasa zaidi ya 100 zilizotolewa pamoja na taarifa ya bodi hiyo, zimedhihirisha kwamba Wolfowitz aliamuru Shaha Riza aongezewe mshahara kufikia karibu dola laki mbili wakati alipohamishwa kufanya kazi katika wizara ya ndani ya Marekani kwa niaba ya benki ya dunia wakati alipochukua hatamu za uongozi katika benki hiyo mnamo mwezi Juni mwaka wa 2005.

Wolfowitz anasema alifuata ushauri wa kamati ya maadili ya benki ya dunia.

´Nilifanya juhudi kufanya nilichofahamu katika ushauri wa kamati ya maadili ya benki ya dunia. Na nilifanya hivyo ili kubeba dhamana kukamilisha jambo nililoamini linaweza kuiharibu taasisi hii.´

Ushahidi mpya unajumulisha kumbukumbu iliyoandikwa na Wolfowitz kwa idara ya huduma za wafanyakazi ya benki ya dunia mnamo mwezi Agosti mwaka wa 2005 ambapo aliiamuru idara hiyo imuongezee mshahara mpenzi wake Shaha Riza.

Wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini Washington, Wolfowitz alijutia kitendo alichokifanya.

´Afadhali kama ningeamini hisia zangu za awali na kujitenga na mazungumzo ya kumuongezea mshahara mkubwa Shaha Riza. Nilifanya makosa ambayo nayajutia na naomba msamaha.

Imefichuka kwamba Shaha Riza ana historia ya kuvunja sheria za benki huku akinufaika kifedha kutokana na kazi zinazohusiana na cheo alichokuwa nacho mpenzi wake Paul Wolfowitz katika wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon.

Kwa mujibu wa shirika la kupambana na ufisadi la Government Accountability Project, GAP, duru za ndani ya benki ya dunia zimedhihirisha kwamba pamoja na Shaha Riza kuongezewa mshahara mkubwa mara mbili katika miaka ya hivi karibuni, hakuwasilisha ombi lolote la kutaka kazi wala kupewa ruhusa ya kufanya kazi na kampuni kubwa ya ulinzi ya Marekani, SAIC, wakati Wolfowitz alipokuwa naibu waziri wa ulinzi.

Katika toleo lake la mwezi Machi gazeti la Vanity Fair liliripoti kwamba Shaha Riza alipokea mishahara kama mtaalamu wa Mashariki ya Kati wa kampuni ya SAIC wakati kampuni hiyo ilipokuwa ikitoa habari za ujasusi kwa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, kabla uvamizi wa Irak mnamo tarehe 19 mwezi Machi mwaka wa 2003.

Shaha Riza alihamishwa kutoka kazi yake kama afisa wa mawasiliano wa benki kuu ya dunia na kupewa kazi kwenye wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, mnamo mwezi Septemba mwaka wa 2005, muda mfupi baada ya Paul Wolfowitz kuchukua hatamu za uongozi wa benki hiyo kuzuia mgongano wa masilahi ya kibinafsi.

Lakini matamshi yake hayakutosha kwa chama cha wafanyakazi wa benki ya dunia kikisema Wolfowitz ameharibu imani ya wafanyakazi na anatakiwa ajiheshimu na ajiuzulu. Katika toleo lake la leo gazeti la Finacial Times pia limemtaka Wolfowitz ang´atuke aidha kwa hiari au atimuliwe na bodi ya magavana.

Wolfowitz anakabiliwa pia na shinikizo kutoka kwa wafanyakazi wenzake kwa mfumo wake wa uongozi kufuatia malumbano kadhaa na bodi ya benki ya dunia kwa kuwapa kazi washirika wake wa chama cha Republican katika benki hiyo. Wolfowitz amesisitiza anngependa kuendelea na kazi yake ili kulifikia lengo la kupunguza umaskini duniani kote.