1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice na Lavrov wakutana

Kalyango Siraj24 Septemba 2008

Suala la Georgia kugusiwa

https://p.dw.com/p/FO3r
Condoleezza Rice, kushoto, na cheo somo wake wa Urusi Sergei Lavrov.Picha: AP

Mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani na Urusi wanakutana jumatano katika kile kinachotarajiwa kuwa 'mkutano wa cheche' kufuatia hatua ya Moscow ya mwezi uliopita ya kutuma vikosi vyake katika nchi jirani ya Georgia.

Uhusiano kati ya Marekani na Urusi umevurugika katika kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita kufuatia hatua ya utawala wa Moscow kutuma vifaru katika eneo la Ossetia Kusini ili kusaidia wapiganaji wanaotaka kujitenga kutoka Georgia.Wapiganaji hao wanaegemea upande wa Urusi.

Na kwa hivyo wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia wanahisi kuwa mkutano utakaofanyika nje ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa, kati ya Bi Condolezza Rice,waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani na cheo somo wake wa Urusi, Sergei Lavrov unatazamiwa kuwa na cheche.

Msemaji wa Bi Condolessa Rice amesema kuwa mazungumzo kati ya mawaziri hao yatajikita katika mpango wa Nuklia wa Iran na Korea Kaskazini.Ameongeza kuwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani,atatumia nafasi hiyo pia kugusia hatua ya kijeshi ya Urusi nchini Georgia.

Yeye msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Marekani, Sean McCormack, akijaribu kupuuza mvutano uliopo amesema kuwa nchi hizi mbili, yaani Marekani na Urusi, zina masuala mbalimbali yanayofanana.

Wasiwasi katika uhusiano kati ya Rice na mwenzake Lavrov umedhihirika wakati wa mikutano kadhaa ya kimataifa iliopita. Katika mikutano hiyo mawaziri hao wawili wamekuwa wakitofautiana katika masuala ya Iran pamoja na mengine. Urusi imekuwa kila mara ikipinga hatua kali dhidi ya Iran.

Kama kuweka bayana msimamo wake katika mkutano wa jumatano wa mjini New York,Urusi imejiondoa katika mazungumzo ambapo mataifa makubwa yalipanga kukutana kesho alhamisi katika duru ya nne kuzungumia vikwazo dhidi ya Iran.Mataifa hayo yanafanya hivyo ,katika hatua ya kuishinikiza Tehran kuachana na mpango wake wa Nuklia.

Rice amekuwa akisimamia uhusiano unaozidi kudorora kati ya nchi yake na Urusi na amekuwa akiongoza hatua za kimataifa za kulaani uamuzi wa Moscow wa kutuma vikosi vya kijeshi nchini Georgia.

Yeye msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Urusi,Andrei Nesterenko amekariri ukosoaji wa nchi yake dhidi ya Marekani ikijaribu kuchanganya ukosoaji wa Moscow na miito ya kuiadhibu Urusi dhidi ya Georgia.