1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice ziarani Mashariki ya Kati

P.Martin1 Agosti 2007

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani,Condoleezza Rice akiwa katika sehemu ya tatu ya ziara yake ya Mashariki ya Kati,hii leo amekutana na waziri mwenzake wa Israel,Tzipi Livni.

https://p.dw.com/p/CHAA
Condoleezza Rice (kushoto) na Tzipi Livni (kulia)kwenye ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem
Condoleezza Rice (kushoto) na Tzipi Livni (kulia)kwenye ubalozi wa Marekani mjini JerusalemPicha: AP

Azma ya ziara ya Waziri Rice katika Mashariki ya Kati ni kuwavutia viongozi wenye siasa za wastani katika kanda hiyo.Vile vile anataka kuanzisha matayarisho ya mkutano wa amani wa Mashariki ya Kati unaotazamiwa kufanywa baadae mwaka huu.

Mkutano huo ulipendekezwa na Rais wa Marekani, George W.Bush katikati ya mwezi Julai,kwa azma ya kufufua majadiliano ya amani kati ya Israel na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas,yaliyokwama tangu muda mrefu.

Mapema leo hii,Waziri wa Nje wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Saud al-Faisal alipozungumza mjini Jeddah kwenye mkutano wa waandishi wa habari pamoja na Rice na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates alisema,nchi yake ipo tayari kuhudhuria mkutano huo wa amani.Akaongezea kuwa itakapopokea mualiko wa kushiriki mkutanoni, italizingatia suala hilo kwa makini na kuhakikisha kuwa itahudhuria mkutano huo wa amani.Mpaka hivi sasa lakini haijulikani ni nani atakaeshiriki katika mkutano huo.Vile vile hata tarehe na mahala pa mkutano bado haijulikani.

Waziri Rice alipoanza ziara yake ya Mashariki ya Kati,alikutana na mawaziri wenzake wa nje kutoka Jordan,Misri na nchi za Ghuba katika mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh nchini Misri siku ya Jumanne.Baadae alipozungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari,Rice alitetea mpango uliopendekezwa na Bush hivi karibuni,kutoa misaada ya kijeshi yenye thamani ya Dola bilioni kadhaa kwa washirika wa Marekani katika Mashariki ya Kati.

Bibi Rice sasa yupo Jerusalem,ambako amekutana na waziri mwenzake Livni.Baadae hii leo anatazamiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel,Ehud Olmert kwenye chakula cha usiku.

Siku ya Alkhamisi,Rice ataelekea Ramallah kwenye Ukingo wa Magharibi kukutana na Rais wa Wapalestina,Mahmoud Abbas na Kaimu Waziri Mkuu Fayyad.Lakini hana mpango wa kwenda Gaza na kukutana na kiongozi wa Hamas,Ismail Haniyeh anaedhibiti Ukanda wa Gaza.

Hii ni ziara ya kwanza ya Rice nchini Israel, tangu mwezi wa Machi na pia ni ya kwanza tangu chama cha Hamas kuuteka Ukanda wa Gaza katika mwezi wa Juni.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel,waziri Rice anatazamiwa kuihimiza Israel kuchukua hatua za kujenga imani zaidi,ambazo zitasaidia kuwaimarisha Abbas na Fayyad.

Lakini haijulikani Olmert yupo tayari kwenda umbali gani kusaidia kumuimarisha Abbas,kiongozi ambae maafisa wa Kiisraeli tangu muda mrefu wamekuwa wakisema kuwa ni dhaifu na hana uwezo wa kuhakikisha usalama na amani.