1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice ziarani nchini Jordan

Josephat Charo26 Machi 2007

Mfalme Abdulla II wa Jordan ameitolea mwito Marekani ihakikishe mazungumzo ya amani ya Mashariki yanafaulu. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, amezuru mjini Amman katika juhudi za kuziunga mkono juhudi za kuufua mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/CHHW
Condoleezza Rice (kushoto) na Mahmoud Abbas
Condoleezza Rice (kushoto) na Mahmoud AbbasPicha: AP

Mfalme Abdullah II wa Jordan amemtolea mwito waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, ahakikishe ufanisi upatikana katika mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati kwa kuzishirikisha nchi zote na kiarabu na dola kuu zinazosimamia mpango wa amani wa aneo hilo. Mfalme Abdullah ameziunga mkono juhudi za Marekani za kutaka kuyafufua tena mazungumzo ya amani baina ya Israel na Palestina.

Condoleezza Rice amefanya mazungumzo na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas mjini Amman Jordan wakati wa mkutano wao wa pili kufanyika kati yao katika kipindi cha saa 24. Baadaye waziri Rice alikutana na mfalme Abdulla II wa Jordan. Rais Abbas amemwambia Condolezza Rice anataka mazungumzo na Israel kuhusu mpango wa amani ya Mashariki ya Kati.

Bi Rice amesema, ´Lazima machafuko yakomeshwe kama kanuni msingi ya amani. Bila shaka haki ya Israel kuwepo lazima itambuliwe. Itakuwa muhimu kuheshimu mikataba iliyofikiwa zamani, na mpango wa Road Map una majukumu ambayo sharti yatimizwe.´

Mpatanishi wa Palestina, Saeb Erakat, amewambaia waandihsi wa habari mjini Amman, Jordan kwamba haitoshi kwa Israel kutaka kuzumgumza na Palestina kuhusu maswala ya misaada ya kiutu na usalama.

Condoleezza Rice anatarajiwa kurejea mjini Jerusalem nchini Israel leo jioni ambako atakutana tena na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert. Maafisa wa Marekani wamesema waziri Rice atawasilisha mpango wa kidiplomasia wa kuyaendeleza mazungumzo ya kutafuta amani baina ya Israel na Palestina yaliyokwama.

Lengo ni kutafuta njia nyengine mbali na mpango uliohusisha pande tatu aliouanzisha waziri Rice mwezi uliopita pamoja na rais Abbas na waziri mkuu Ehud Olmert. Condoleezza Rice anatarajiwa kuutangaza mpango huo mpya wakati atakapokutana na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Ehud Olmert mjini Jerusalem.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema mjini Jerusalem kwamba waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert atakuwa tayari kuhudhuria mkutano na viongozi wa mataifa ya kiarabu yasiyo na msimamo mkali wa kidini iwapo ataalikwa.

Akitoa ushauri kwa serikali mpya ya kitaifa ya mamlaka ya Palestina, Ban Ki Moon ameongeza kusema, ´Pande nne zingependa kuiona serikali hii ikijitolea wazi kukomesha machafuko, kuitambua Israel na ikubali mikataba iliyofikiwa hapo awali. Hatua nyengine muhimu kwa serikali mpya ni kuchukua hatua dhidi ya kuvurumishwa kwa maroketi kutoka Gaza na kuachiliwa kwa mwanajeshi wa Israel, koplo Gilad Shalit.´

Juhudi za Marekani kuyafufua mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati yalisambaratika wakati chama cha Fatah cha rais Mahmoud Abbas kilipoungana na chama cha Hamas kuunda serikali ya umoja wa kitaifa mwezi uliopita. Marekani na washirika wake wa kimataifa wameigomea serikali ya mamlaka ya Palestina kwa hatua ya chama cha Hamas kukataa kukomesha machafuko na kuitambua Israel.

Ili kuondoa hali ya kutoaminiana iliyosababishwa na serikali hiyo ya umoja wa kitaifa, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, amekuwa akitafuta uungwaji mkono miongoni mwa mataifa ya Warabu wa madhehebu ya Sunni kama Jordan kuishawishi Israel ikubali kurejea tena katika mazungumzo.

Mjini Riyadh Saudi Arabia, mawaziri wa mashauri ya kigeni wa mataifa ya kiarabu wameidhinisha mpango wao wa amani ulioandaliwa miaka mitano iliyopita.