1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silaha zilizotumiwa na IS zilitoka nchi za Umoja wa Ulaya

Isaac Gamba
15 Desemba 2017

Zaidi ya theluthi moja ya silaha zilizotumiwa na kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu, IS nchini Iraq na Syria zilitoka katika mataifa ya Umoja wa Ulaya ikiwa ni pamoja na Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2pQD2
Irak Kirkuk Kurden-PKK
Picha: picture-alliance/AA

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyochapishwa jana kuhusu uchunguzi yenye kurasa 200 ya shirika hilo linalofuatilia masuala ya silaha zaidi ya asilimia 30 ya silaha zlizotumiwa na kundi la Dola la Kiisilamu, IS katika mapigano nchini Syria na Iraq ziliuzwa kutoka katika viwanda vya silaha nchini Bulgaria, Romania, Hungary na Ujerumani.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa Urusi na China zilitengeneza zaidi ya nusu ya silaha hizo zilizotumiwa na kundi hilo la kigaidi.

Utafiti wa shirika hilo la CAR ulifanywa katika kipindi cha miaka mitatu nchini Iraq na Syria na umeonesha kuwa silaha kali zinaweza kutumbukia katika mikono isiyo salama.

Katika kipindi cha kati ya mwaka 2014 na 2017 watafiti waliohusika na utafiti huo walichunguza zaidi ya silaha 40,000 zilizopatikana katika maeneo ya mapigano ya kundi la IS ikiwa ni pamoja na bunduki, risasi na vifaa vingine vinavyotumika kutengeneza milipuko.

Silaha hizi ziliporwa kutoka kwa wapiganaji wa vikosi vya serikali

Ripoti hiyo inaeleza kwamba silaha nyingi zilizotumiwa na kundi la IS ziliporwa kutoka kwa wapiganaji wa vikosi vya serikali vya Iraq na Syria lakini hata hivyo silaha zilizonunuliwa na mataifa ya Saudi Arabia na Marekani na baadaye kusambazwa kwa vikosi vya makundi ya upinzani nchini Syria nazo pia zilitumbukia mikononi mwa kundi hilo la Dola la Kisilamu.

Utafiti huu unakumbusha juu ya mkanganyiko uliopo unaotokana na usambazaji wa silaha katika maeneo yenye mizozo ambako makundi kadhaa yakiwemo yasiyo ya serikali yanashiriki katika mapigano.

Halbautomatische Waffe
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Breed

Ripoti hii inaelezea jinsi Saudi Arabia na Marekani zilivyonunua silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola  kutoka mataifa ya Ulaya Mashariki kabla ya kuzigawa silaha hizo kwa makundi ya upinzani nchini Syria na mara nyingi wakifanya hivyo kwa kukiuka makubaliano yanayohusisha manunuzi ya silaha hizo.

Ripoti hiyo imefafanua kuwa usambazaji wa silaha hizi umekuwa ukikiuka makubaliano ya manunuzi kati ya muuzaji ambayo ni nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya na mnunuzi Saudi Arabia na Marekani. 

Kwa upande mwingine shirika hilo limebaini juu ya silaha za kisasa zilizo na uwezo wa kuzuia mashambulizi ya vifaru zilizotengenezwa na nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya ambazo zimeuzwa nchini Marekani na baadaye kusafirishwa nchini Syria kabla ya silaha hizo kuishia mikononi mwa wanamgambo wa IS nchini Iraq ikiwa ni ndani ya miezi miwili tangu silaha hizo zitoke kiwandani.

Kwa mujibu wa shirika la CAR pande zinazohusika na mchakato huu wa usafirishaji wa silaha mara nyingi kwa makusudi kabisa zimekuwa zikijaribu kubadilisha maelezo yanayoonesha silaha zilikotoka kwa kubadilisha utaratibu wa kufungasha silaha hizo ama kufuta alama za kiwanda zilikotengenezwa.

Mwandishi: Isaac Gamba/Reuters, http://bit.ly/2C9NCVz

Mhariri: Grace Patricia Kabogo