1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya jenerali Petreaus yakataliwa na wabunge

Josephat Charo12 Septemba 2007

Wabunge wa vyama vya Democratic na Republican nchini Marekani wameikataa ripoti ya kamanda mkuu wa jeshi la Marekani nchini Irak.

https://p.dw.com/p/CB1K
Jenerali David Petraeus
Jenerali David PetraeusPicha: AP

Wabunge wenye ushawishi mkubwa wa vyama vya Democtratic na Republican nchini Marekani wameikataa ripoti iliyotolewa na kamanda mkuu wa jeshi la Marekani nchini Irak, David Petreaus inayotathimini hali nchini Irak.

Jenerali Petreaus na balozi wa Marekani nchini Irak, Ryan Crocker, wamekabiliwa na malalamiko ya wabunge kwamba hatua ya kuongeza idadi ya wanajeshi nchini Irak imeshindwa kutimiza lengo lake kubwa la kuleta upatanisho wa kisiasa.

Mgombea wa urais wa chama cha Democratic, Barack Obama, amesema ni makosa kuiwasilisha ripoti kuhusu hali nchini Irak katika siku iliyojaa huzuni ya shambulio baya zaidi la kigaidi kuwahi kufanywa duniani akisema kufanya hivyo ni kujaribu kudhihirisha kwamba uamuzi wa kwenda vitani nchini Irak unahusiana na mashambulio ya Septemba 11 mwaka wa 2001 nchini Marekani.

Aidha Barack Obama amesema, ´Tumeweka sasa kipimo kuw achini mno kiasi cha kuuita ufansi katika hali iliyo mbaya kabisa. Imefikia kiwango ambapo sasa machafuko mengi yasoweza kuvumilika yaliyokuwepo mwezi Juni mwaka jnana wa 2006 yanaelezwa kuwa ufanisi. Na si hivyo. Hili linaendelea kuwa kosa kubwa la sera ya kigeni.´

Mbunge wa chama cha Democratic, Joseph Biden amesema juhudi za Marekani nchini Irak zimeshindwa hivyo kutofautiana na matamshi ya jenerali Petreaus aliyesisitiza ufanisi umepatikana nchini Irak.

Chama cha Democratic kimesema mkakati mpya wa jenerali Petraeus unaashiria miaka mingine kumi ya vita nchini Irak huku rais George W Bush akitarajiwa kulihutubia taifa hii leo katika ikulu yake mjini Washington.