1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Marekani juu ya nuklia,Iran yasema ni ushindi kwake

6 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CXiH

TEHRAN.Rais Mahmoud Ahmednejad amesema kuwa ripoti iliyotolewa na idara za ujasusi za Marekani juu ya mpango wake wa nuklia, ni ushindi mkubwa kwa nchi yake.

Hapo siku ya Jumatatu idara hizo katika taarifa ya pamoja zilisema kuwa Iran ilisitisha mpango wa kutengeza silaha za nuklia toka mwaka 2003.

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni Rais huyo wa Iran amesema kuwa ripoti hiyo ni pigo kubwa kwa wale ambao kwa miaka kadhaa wameigubika dunia kwa vitisho na shinikizo.

Rais Ahmednejad akaonya kuwa yoyote atakayetaka kuanzisha mzozo mpya na nchi hiyo wananchi wa Iran watajibu vikali na kamwe hawatarudi nyuma.

Amesema kuwa Iran iko tayari kuupokea mkono wa majadiliano utakayooshwa kwao kiurafiki na si kama adui.

Rais Bush mapema alisisitiza kuwa Iran bado ni tishio na akasema ni lazima itimize masharti ya Umoja wa Mataifa kabla ya kwenda katika meza ya majadiliano.

Kwa upande mkuu wa Shirika la kimataifa la Atomic Mohamed El Baradei akizungumza mjini Brasilia Brazil amesema kuwa ripoti hiyo imeisafisha Iran na kwamba inatoa nafasi mpya kwa wanadiplomasia katika suala hilo.

Mjini Washington Makamu wa Rais wa Marekani Dicky Cheney amekiri kuwa ripoti hiyo inaweza kukwaza harakati za kidiplomasia za nchi hiyo katika suala la Iran.