1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Marekani kuhusu Haki za Binaadam Duniani

12 Machi 2010

<p>Kila mwaka,Marekani hutoa ripoti yake kuhusu hali ya haki za binadamu kote duniani.China,Iran,Cuba,Korea ya Kaskazini na Sudan ni nchi zilizokosolewa zaidi katika ripoti iliyowasilishwa siku ya Alkhamisi.

https://p.dw.com/p/MQuv
Secretary of State Hillary Rodham Clinton speaks during her joint news conference with Yemen's Foreign Minister Abu Bakr al-Qirbi, not shown, Thursday, Jan. 21, 2010, at the State Department in Washington. (AP Photo/Luis M. Alvarez)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,Hillary Clinton.Picha: AP

Ripoti ya mwaka 2009, iliyowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton, mjini Washington, inaeleza juu ya hali ya haki za binadamu katika nchi 194. Mkuu wa kitengo kinachoshughulikia masuala ya haki za binadamu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Michael Posner, amesema si wote wanaoipenda ripoti hiyo, lakini inasomwa na kila mmoja. Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya, ukiukaji wa haki za binadamu umeongezeka katika nchi nyingi, lakini vile vile kunafanywa jitahada nyingi zaidi kupambana na tatizo hilo. Ripoti hiyo ni msingi mmojawapo muhimu katika sera za nje za Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje, Hillary Clinton, akiwasilisha ripoti hiyo, amesema:

"Amani haiwezi kupatikana bila ya kuheshimiwa haki za kimsingi za kila binaadam."

China, Iran, Cuba, Korea ya Kaskazini na Sudan ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika orodha ya mataifa yaliyokosolewa vikali kwa ukiukaji wa haki za binadamu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hakuna maendeleo yaliyopatikana nchini China kuhusu haki za binadamu, bali hali imezidi kuwa mbaya. Nchini humo wapinzani wa serikali wanazidi kusumbuliwa na hata makundi ya kitamaduni na kabila ya wachache yanaendelea kukandamizwa.

Iran nayo imekosolewa kwa hatua kali zinazochukuliwa na serikali dhidi ya waandamanaji.Na Cuba kwa sababu ya hali mbaya inayokutikana katika jela zake na wafungwa wanaofariki kwa sababu ya kugoma chakula. Lakini wataalamu katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani wana wasiwasi pia na baadhi ya matukio barani Ulaya. Michael Posner anasema:

"Waislamu wanazidi kubaguliwa na kuna visa vya chuki." 

Miongoni mwa mambo aliyokosoa ni kupigwa marufuku ujenzi wa minara ya msikiti nchini Uswisi, kama wananchi wake walivyotaka katika kura ya maoni iliyopigwa. Hata Ujerumani imetajwa katika ripoti hiyo.Michael Posner akifafanua anasema:

"Mfumo wa sheria wa Ujerumani ni imara, lakini kuna ila pia -  kama vile ubaguzi." 

Kwa mfano ,Kanisa la Scientology linalochunguzwa; au waalimu wa Kiislamu wanaokatazwa kuvaa hijabu darasani. Ripoti hiyo inaongezea kuwa chuki dhidi ya wageni na Wayahudi, ni matatizo yaliyoenea Ujerumani. Wakati huo huo inasema kwamba uhuru wa Wanazi mamboleo na makundi mengine yenye sera kali za mrengo wa kulia, kueleza maoni yao unawekewa vizuizi.

Na barani Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria na Sudan ni nchi zilizotajwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadam - na hayo yote ni maeneo ya migogoro.

Muandishi: Müller,Sabine/ZPR/ P.Martin

Mhariri: Othman,Miraji

Audio in DaletWeb:

Ende