1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Shirika la Amnesty International

Othman, Miraji28 Mei 2008

Katika ripoti ya Shirika la Amnesty International linalotetea haki za binadamu duniani iliotolewa leo, Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya zimelaumiwa vikali.

https://p.dw.com/p/E7fM
Bibi Irene Khan, katibu mkuu wa Shirika la Amnesty International la kupigania haki za binadamu dunianiPicha: AP

Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini London limezitaja nchi kadhaa kwa kwenda kinyume na haki za binadamu, ikiwemo China ambayo inaendelea kudharau mapendekezo ya Tangazo hilo la kimataifa ambalo mwaka huu linaadhimisha mwaka wake wa 60 tangu kutolewa.

Shirika la Amnesty limesema viongozi wa dunia inawabidi waombe radhi kwa kushindwa kutekeleza ahadi ya kuleta haki na usawa duniani. Katika ripoti hiyo ya mwaka ya Amnesty International kumetajwa visa mbali mbali vinavokwenda kinyume na maagizo ya Tangazo hilo la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu ambalo lilitolewa Disema 10, mwaka 1948. Amnesty International imesema bado watu wanateswa au kutendewa vibaya katika nchi 81, wanakabiliwa na mashtaka yasiokuwa ya haki katika nchi 54 na hawana uhuru wa kuelezea maoni yao katika nchi 77, licha ya kwamba nchi hizo zinatakiwa ziishi chini ya maagizo ya tangazo hilo la kimataifa.

Ililiuliza kama Umoja wa Ulaya au nchi zanachama za Umoja huo zinaweza kutoa miito kutaka haki za binadamu ziheshimiwe na nchi kama Russia na Uchina wakati nchi hizo hizo za Umoja wa Ulaya zenyewe zinashirika katika kuwatesa watu? Ripoti hiyo ilikuwa inaashiria juu ya madai kwamba baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zilikubaliana na mipango ya Marekani ya kuwatesa katika nchi zao watu waliokuwa vizuizini. Nchi za Umoja wa Ulaya ziliulizwa na ripoti hiyo kama kweli zinaweza kuhubiri juu ya uvumilivu na ustahamilivu wakati nchi hizo zimeshindwa kupambana na ubaguzi dhidi ya Magipsy, Waislamu na watu wengi walio wa jamii za wachache wanaoishi ndani ya nchi zao? Kwa vile Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya zinajikwaa katika rikodi zao kuhusu haki za binadamu, uwezo wa nchi hizo kuzishawishi nchi nyingine unapungua.

Serikali ya Marekani imelaumiwa kwa kuzidhoofisha sheria zinazopiga marufuku watu kuteswa, kushindwa kuwajibika majeshi yake huko Iraq, na kumuunga mkono Rais Musharaaf wa Pakistan pale alipowakamata maelfu ya wanasheria, waandishi wa habari, wanaharakati wa haki za binadamu na watetezi wa demokrasia, utawala wa sheria na mahakama zilizo huru. Ilielezewa matarajio kwamba Marekani italifunga gereza lake la Guantanamo.


Uchina nayo ililaumiwa kwa kupeleka silaha Sudan licha ya marufuku iliowekwa na Umoja wa Mataifa, pia kuupa silaha utawala wa kijeshi wa Myanmar. Katibu Mkuu wa Amnesty Interrnational Irene Khan alikuwa na haya ya kusema juu ya serekali ya Uchina ambayo mwaka huu ni mwenyeji wa michezo ya Olympik...

+China ilitoa ahadi kwamba pindi michezo ya Olympik itafanyika katika nchi yake, bila ya shaka itafanya mabadiliko ili kutekeleza haki za binadamu. Tunataka China itekeleze ahadi hiyo. Kuna maendeleo kidogo kuhusu suala la hukumu za vifo, lakini kuna mengi yasiofanywa bado. Kabla ya michezo ya Olympik kumeengezeka visa vya kuendewa kinyume haki za binadamu. Iko haja ya kuboresha hali ya mambo, pia baada ya michezo ya Olympik. Dunia inailengea China kama nchi hiyo inayokuwa dola kuu la dunia itawajibika katika masuala ya haki za binadamu kama nchi nyingine.+

Amnesty International ilikuwa na wasiwasi kuhusu hali ya mambo hujko Zimbabwe ambako vitendo vya utumiaji nguvu vimezidi na watu 22 kuuwawa baada ya uchaguzi wa bunge na rais uliopita. Serekali ya Rais Mugabe wa nchi hiyo ilitakiwa iuendeshe uchaguzi ujao wa urais hapo Juni 27 kwa njia ya amani na iwaruhusu waangalizi wa kimaitaifa wa uchaguzi huo waingie nchini.