1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhalifu uliofanywa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kati ya mwaka 1993 na 2003

Oumilkher Hamidou1 Oktoba 2010

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa mataifa kuhusu haki za binaadam bibi Navi Pillay aashauri ripoti hiyo idurusiwe kwa makini

https://p.dw.com/p/PSHR
Wakinamama mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo

Umoja wa mataifa umetangaza hii leo ripoti inayofafanua uhalifu uliofanywa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kati ya mwaka 1993 na 2003-hati inayokosolewa vikali na Rwanda na Uganda zinazotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.

Katika taarifa yake, mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binaadam bibi Navi Pillay ameanza kwa kuzungumzia mjadala mkali ulioripuka baada ya "kufichuliwa hati hiyo mwishoni mwa mwezi wa Agosti mwaka huu, lakini anasema "mjadala huo ulituwama katika mada moja tuu-yaani uwezekano wa kwamba vikosi vya jeshi la Rwanda na washirika wao wa kienyeji pengine wamefanya visa vinavyoweza kulinganishwa na mauaji ya halaiki."

"Ripoti inasisitiza suala hilo haliwezi kufafanuliwa isipokuwa katika mahakama maalum tuu"-ameongeza kusema mwenyekiti huyo wa halmashauri kuu ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binaadam. Bibi Pillay amezungumzia umuhimu wa ile hali kwamba ripoti hiyo inaihusu Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo pamoja na visa vilivyofanywa na mataifa jirani katika nchi hiyo."

Ikiwa ni matokeo ya utafiti wa mwaka mzima, kuanzia Julai mwaka 2008 hadi June 2009, ripoti hiyo ya kurasa 550 inachambua visa 617 vya uhalifu wa hali ya juu uliogharimu maisha ya maelfu ya raia kati ya mwaka 1993 hadi 2003 katika ile iliyokuwa ikijulikana zamani kama Zaire na hasa katika kipindi cha mwaka 1996 hadi 2001.

Bibi Pillay amezungumzia umuhimu wa kutathminiwa kwa makini ripoti hiyo na hasa hatua zilizoshauriwa ili waasisi wa visa hivyo wakajieleze mahakamani. Bibi Pillay amesema anaamini mamilioni ya wahanga wa uhalifu huo hawastahiki kitu chengine badala ya hicho."

Serikali ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo inadai "haki" kwa wahanga wa visa hivyo vya uhalifu" amesema hayo balozi wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo katika Umoja wa mataifa Ileka Atoki." Ripoti hiyo ni timamu na ni ya kuaminika-ingawa yaliyomo yanajulikana tangu zamani-"amesema na kusisitiza wahanga wa Kongo wanastahiki sauti yao isikilizwe.

"Ripoti hiyo ni mbaya na ni ya hatari kuanzia mwanzo mpaka mwisho" amesema kwa upande wake waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda, Luise Mushikiwabo, katika taarifa iliyolifikia shirika la habari la Ufaransa, AFP.

Ripoti hiyo imekosolewa kikamilifu na Uganda pia inayosema imeandaliwa kutokana na uvumi na uwongo na bila ya misingi yoyote.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo