1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robert Enke aombolezwa.

11 Novemba 2009

Rambi rambi nyingi kwa kipa wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/KU47
Marehemu Robert EnkePicha: picture-alliance / augenklick/RO

Kipa wa timu ya Taifa ya Ujerumani na wa klabu ya Bundesliga (Hannover 96) Robert Enke, aliejiua jana jioni, akisumbuliwa na maradhi ya kimawazo.Taarifa hiyo ametoa leo daktari wake,Valentin Markser mjini Hannover.

Robert Enke,aliekuwa na umri wa miaka 32, aliaga dunia jana jioni katika kitongoji cha Hannover cha Rübenberge baada ya kujiachia kugongwa na gari-moshi kivukoni.DFB-shirikisho la dimba la Ujerumani limevunja mechi ya kirafiki ya jumamosi na Chile mjini Cologne.

"Naweza kuthibitisha leo asubuhi imegunduliwa barua ya kuaga dunia marehemu,lakini kwa kuifikiria familia yake na hata yeye mwenyewe marehemu Robert Enke hatungependa kufichua zaidi yaliomo".-alieleza daktari wake.

Hatahivyo, imefahamika kwamba, katika barua hiyo, marehemu aliomba radhi tangu kwa daktari wake hata kwa familia yake na jamaa zake kwa uamuzi aliochukua wa kujiua.

Kwa muujibu wa kizuka wake bibi Teresa, marehemu akisumbuliwa sana na majonzi na mawazo mengi."Nilitaka sana kumsaidia katika mitihani yake hadi apone."Aliuwambia mkutano na waandishi habari leo huku akichuchurikwa na machozi.Akaongeza, Robert lakini alikataa kwenda katika hazanati kutibiwa ."Mume wangu akihofia kumpoteza mtoto wao wa kulea Leila.Hata siku ile ya kifo chake, daktari wake alinasihi Robert kuingia hospitali atibiwe,lakini alikataa.

Stadi huyu wa dimba na mlinzi wa lango la Hannover 96 katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani, alifiwa na mtoto wake wakike wa miaka 2 kwa maradhi ya moyo aliozaliwa nayo.Kitoto hicho kilikua mapenzi yake makubwa.Mei mwaka huu akamamua kumlea Leila.

Daktari wa marehemu, Valentin Markser, alisema kuwa,ukubwa wa maradhi yake ya fikra na mawazo ulipofikia ,mara nyingi humalizikia hatima kama hiyo .

Kifo cha Robert Enke, kimeustusha ulimwengu wa dimba na sio tu mjini Hannover, Ujerumani nzima bali hata nje yake.Klabu yake alioichezea zamani FC Barcelona, iliomboleza jana kifo chake.

Mashabiki mamia kadhaa wa timu yake ya Hannover 96-klabu ya daraja ya kwanza ya Bundesliga nao wameomboleza. Shabiki mmoja alisema:

"Alikuwa kipenzi chetu cha kupigiwa mfano, ni kipenzi sio kila mmoja huwanacho.Ni mara moja tu hupatikana."

Huku wingu la huzuni likigubika dimba la Ujerumani na Shirikisho la dimba la Ujerumani DFB kuamua kuivunja mechi yake na Chile mjini Cologne, Jumamosi hii, rambi rambi zimeanza kumiminika: Sepp Blatter, rais wa FIFA amesema, "Fikra zetu zote katika kipindi hiki kigumu ziko kwa mkewe na ukoo wake Robert Enke.Tunakutakia nguvu kuhimili majonzi na machungu."

Rais wa Shirikisho la dimba la Ujerumani DFB,Theo zwanziger alisema:

"Tumeduwaa ! hatuna la kusema,tumejaa huzuni..." Nae Beckenbauer, mfalme wa dimba wa Ujerumani alisema, "Nina huzuni kubwa kusikia taarifa kama hiyo".

Mwandishi: Ramadhan Ali/EPD/SID

Mhariri: Abdul-Rahman