1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robert Mugabe ,mpigania uhuru aliyegeuka kuwa dikteta

Sekione Kitojo16 Aprili 2010

Kesho Jumapili Zimbabwe inasherehekea miaka 30 ya uhuru kutoka Uingereza. Nchi hiyo ilikuwa mfano wa mafanikio katika bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/Myg4
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akitoka katika mkutano na rais wa Afrika kusini Jacob Zuma mjini Harare.Picha: AP

Kesho Jumapili tarehe 18 April , Zimbabwe inasherehekea miaka 30 ya uhuru. Nchi hiyo ilikuwa mfano wa mafanikio katika bara la Afrika. Kiongozi wake , Robert Mugabe , alikuwa maarufu sana katika mataifa ya magharibi. Kutoka katika kasri la malkia mjini London hadi katika ikulu ya Marekani mjini Washington , kila mahali Mugabe alipokwenda , viongozi wa mataifa ya kigeni walimsifu kwa juhudi zake za kupambana na umasikini na kufanya mapatano kati ya Waafrika na Wazungu nchini Zimbabwe. Lakini latika miaka ya hivi karibuni , Mugabe amekuwa akitengwa na mataifa ya magharibi. Taarifa yake Chiponda Chimbelu juu ya shughuli za mpigania uhuru huyu ambaye amekuwa sasa dikteta inasomwa studioni na Sekione Kitojo.

Umati wa watu ulishangilia , wakati Robert Mugabe alipochukua madaraka kama waziri mkuu wa Zimbabwe mwaka 1980. Katika miaka ya nyuma, Zimbabwe ambayo ilikuwa inajulikana kama Rhodesia, imekuwa ikitawaliwa na serikali ya Wazungu wachache. Ukandamizaji wa kinyama dhidi ya Waafrika waliowengi ilikuwa hali ya kawaida kila siku. Waafrika na Wazungu nchini Zimbabwe walipigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Baada ya vita kumalizika na Robert Mugabe kuchukua madaraka , watu walimuona kama mkombozi. Martin Meredith alizaliwa nchini Afrika kusini, na akiwa mwandishi habari maarufu na mwandishi vitabu, aliandika vitabu kadha juu ya historia ya Afrika.

Ni kweli wakati Mugabe alipochukua uongozi katika mwaka 1980, alikuwa mmoja wa viongozi walioheshimiwa sana katika bara la Afrika. Ilikuwa ni kwasababu kwa upande mmoja baada ya miaka saba ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, aliahidi kuleta masikilizano baina ya Waafrika na Wazungu ambao hapo zamani waliitawala Zimbabwe. Kwa miaka kadha , katika miaka ya 1980, uhusiano wa Mugabe na Wazungu ulikuwa mzuri tu.

Tofauti na viongozi wengine wa Afrika, Mugabe hakuchukua sera za kuwawezesha Waafrika. Kwa mfano aliruhusu wakulima wa Kizungu ambao walikuwa wakimiliki mashamba makubwa kubakia katika mashamba hayo. Mpango wa mageuzi ya ardhi ulitumika kwa msingi wa yule aliyetaka kuuza ardhi yake na yule aliyetaka kununua. Kwa hiyo aliweza kuwabakisha Wazungu ambao wana ujuzi. Hata wapinzani wake walisifu juhudi zake za kupanua sekta za elimu na afya. Lakini mambo yalianza kugeuka . Heidi Holland ni mtunzi wa kitabu Dinner with Mugabe, kula chakula la usiku na Mugabe, ambacho ni juu ya maisha ya kiongozi huyo wa Zimbabwe.

Moja ya nyakati muhimu, ni wakati wapigakura Wazungu nchini Zimbabwe ambao walikuwa na uhakika wa kuwa na viti katika bunge chini ya makubaliano ya katiba ya Lancaster House, ambayo imepatikana kutokana na upatanishi wa Uingereza ambayo ilikuwa mkoloni wa zamani wa Zimbabwe, walipopiga kura kumuunga mkono Ian Smith, waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, na adui mkubwa wa Mugabe, badala ya kumpigia kura Mugabe, ama hata baadhi yao wangempigia Mugabe wakati akijaribu kwa nguvu zote kuwakumbatia. Nafikiri ukweli kwamba Wazungu walipiga kura kwa misingi ya kibaguzi hii ndio ilikuwa wakati mambo yalipobadilika.

Kwa mtazamo wa Holland, Mugabe alikasirishwa na Wazungu . Katika mtazamo wa Holland, Mugabe alianza kuingiwa na hasira dhidi ya Wazungu . Kwa maoni yake , walipaswa kuwa waaminifu kwake, anasema Holland. Kwa mtazamo wake, Mugabe alifikiri kuwa anastahili heshima kwa kuwaruhusu kubakia nchini Zimbabwe, hata kama serikali ya Wazungu wachache ilimtesa na kumfunga jela kwa muda wa miaka 11. Heidi Holland anafikiri kuwa hatua alizochukua Mugabe dhidi ya wakulima wa Ki kwa kiasi fulani ni kutokana na matumizi ya nguvu na kisaikolojia ambayo yeye pamoja na Waafrika wengi walikumbana nayo wakati wa utawala wa Wazungu.

Mwandishi: Chimbelu, Chiponda (DW Intern)/Sekione Kitojo

Mhariri: Josephat Charo