1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ROMA: Mtekajinyara wa ndege ya abiria ajiwasilisha kwa polisi

4 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD6P

Kisa cha utekaji nyara wa ndege ya abiria ya shirika la ndege la Uturuki kimemalizika. Ndege hiyo iliyokuwa imewabeba abiria 107 ilikuwa njiani ikielekea Istanbul kutoka Albania, wakati mwanamume mmoja ambaye hakuwa na silaha alipoingia chumba cha marubani na kuwaamuru wailekeze ndege hiyo kwenda Roma, Italia.

Lakini wafanyakazi wa ndege hiyo walitoa habari kisiri wakiashiria kutekwa nyara. Mara moja ndege za kivita za Italia ziliifuata ndege hiyo na kuilazimisha itue katika mji wa Brindisi, kusini mwa Italia, ambako mtekaji nyara huyo alijiwaslisha kwa polisi.

Polisi wanaamini mwanamume huyo alikuwa peke yake, lakini wanachunguza ripoti kwamba huenda alikuwa na mwenzake katika njama hiyo.

Maofisa wa Italia na Uturuki wanasema mwanamume huyo aliwacha kazi yake katika jeshi la Uturuki na alikuwa akitafuta ukimbizi nchini Italia.

Maofisa wamekanusha madai kwamba utekaji nyara wa ndege hiyo ya abiria ni kitendo cha kupinga ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki, baba Mtakatifu Benedict XVI nchini Uturuki mwezi Novemba mwaka huu.