1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Romney aahidi kuirejeshea Marekani hadhi yake

31 Agosti 2012

Mgombea wa urais nchini Marekani kupitia chama cha Republican Mitt Romney ameapa kuirejeshea Marekani nafasi yake ya uongozi wa dunia atakapochaguliwa kuwa rais hapo Novemba 6.

https://p.dw.com/p/161Ka
Mitt Romney akiwapunguia wanachama wa Republican wakati akipanda jukwani kukubali uteuzi.
Mitt Romney akiwapunguia wanachama wa Republican wakati akipanda jukwani kukubali uteuzi.Picha: Reuters

Kupandishwa kwa Romney kuwa mshindani rasmi wa rais Barack Obama katika uchaguzi wa Novemba kumekuja zaidi ya miaka mitano baada ya jaribio lake la kwanza kuingia Ikulu ya White House na huku mchuano kati yao ukionekana kuwa mkali zaidi na ushindi ukitegemea majimbo machache muhimu kama vile Florida, Ohio, Virginia na Colorado ambayo lolote kati yake linaweza kuamua mshindi. Baada ya kuwa nyuma ya rais Obama kwa miezi kadhaa, tajiri Romney amepunguza pengo kati yake na Obama ambaye anakabiliwa na suala la uchumi mbaya na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira.

Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi wa chama hicho kuwa mgombea wake wa urais, Romney alisema Marekani inachotaka hivi sasa ni ajira kwa wingi na kuongeza kuwa rais Barack Obama ameshindwa kutekeleza ahadi zake. "Natamani rais Obama angefanikiwa kwa sasabu nataka Marekani ifanikiwe, lakini ahadi zake zimesababisha kuvunjika mioyo, na hili ndilo jambo tunalopaswa kukubali. Sasa ndiyo wakati ambapo tunaweza kufanya kitu, na kwa msaada wenu tutafanya kitu," alisema Romney huku akipigiwa nderemo na vifijo.

Paul Ryan, mgombea mwenza wa Mitt Romney.
Paul Ryan, mgombea mwenza wa Mitt Romney.Picha: dapd

Atumia ufanisi wake kibiashara kama kigezo
Romney amejipigia debe kwa kutumia welekevu wake wa kibiashara, na kusema kuwa ana ujuzi unaotakiwa kuiondoa Marekani katika mkwamo wa kiuchumi na kuipeleka katika mafanikio, huku akiahidi kuunda ajira mpya milioni 12 na kuifanya Marekani kuwa taifa linalojitegemea katika nishati ifikapo mwaka 2020. Lakini gavana huyo wa zamani wa Jimbo la Massachusetts anashindwa vibaya kimvuto na Obama. Kazi ya kuongeza umaarufu wa Romney imemuangukia mke wake Ann, ambaye alitoa hotuba iliyowasisimua wengi siku ya Jumanne kuhusu mapenzi yake na Romney wakiwa wanafunzi, familia yao ya Kimarekani na upendo wake wa kuitumikia jamii.

Katika kilele cha siku tatu za mkutano huo wa chama cha Republican, zilitolewa hotuba mfululizo na kupandishwa jukwani watu mbalimbali maarufu, katika kile kilichoonekana kama kujaribu kumtambulisha upya Mitt Romney kama mtu wa watu zaidi. Mtoto wake Craig alifuatiwa na waumini wa Kanisla lake la Mormon, washiriki wa mashindano ya Olimpiki na msanii wa siku nyingi wa Hollywood, Clint Eastwood, ambao wote walikuwa na kazi ya kuushambulia utawala wa rais Barack Obama. Wachambuzi wameilezea hatua ya Eastwood ya kuzungumza na kiti kitupu akikifaananisha na rais Obama kuwa kosa la kisiasa lililofanywa na timu ya kampeni ya Romney.

Ann Romney, mke wa Mitt Romney akizungumza wakati wa siku ya pili ya mkutano wa chama cha Republican.
Ann Romney, mke wa Mitt Romney akizungumza wakati wa siku ya pili ya mkutano wa chama cha Republican.Picha: Reuters

Watoa ushuhuda jinsi alivyowasaidia
Familia moja ya waumini wa kanisa lake ilitoa ushuhuda wa jinsi Romney alivyomsaidia mtoto wao aliyekuwa anaumwa na ugonjwa wa saratani, ikiwa ni pamoja na kumsaidia kuandika wosia. Lakini Romney mwenyewe hakuzungumzia imani yake kwa undani, aina ya ukristo ambao wengi hawauamini lakini hotuba yake ilikuwa na visa binafsi vilivyolenga kumsaidia kuwafikia Wamarekani wa daraja la kati.

Jambo kubwa lililosisitizwa katika hotuba ya Romney, ni kuwa rais Barack Obama alipewa nafasi na kwamba ameshindwa na hivyo wakati umefika achaguliwe mtu ambaye anaweza kubadilisha mambo. "Kaulimbiu za matumaini na mabadiliko zilikuwa na ushawishi mkubwa kwenu. Lakini usiku huu ningependa niwaulize swali moja; Kama mlipata furaha mlipomchagua Barack Obama, hampaswi kujiskia hivyo sasa hivi kwa vile yeye ni rais?," aliuliza Romney.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, dpae, rtre
Mhariri: Josephat Charo