1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rousseff ajitetea kumteua Lula kuwa Mkuu wa Ofisi yake

Yusra Buwayhid17 Machi 2016

Rais wa Brazil Dilma Rousseff amemteua rais wa Zamani Luiz Inacio Lula da Silva kuwa Mkuu wa Ofisi yake, uamuzi unaotajwa kuwa ni njia ya kumlinda kufunguliwa mashitaka kwa madai ya kuhusiaka na makosa ya ufisadi.

https://p.dw.com/p/1IETj
Brasilien Protest Anti Rousseff
Picha: picture-alliance/dpa/R. Nogueira

Katika mji mkuu wa Brasilia, zaidi ya waandamanaji 5,000 wamekusanyika nje ya jengo la baraza la congress huku polisi wakijaribu kuwatawanya. Waandamanaji hao wanaonekana wakiwa wameshika mabango yenye maandishi yanayomtaka rais wao - mfuasi wa siasa za mrengo wa kushoto - ajiuzulu na Lula akamatwe.

Maelfu ya watu wengine wameandamana katika barabara kuu ya Paulista ya mji wa kibiashara wa Sao Paulo, mji uliokuwa na maandamano mengine ya karibu watu milioni moja waliokuwa wakimtaka Rais huyo ajiuzulu Jumapili iliyopita.

Aidha Rousseff alijitetea kwa kusema alimteua Lula kuwa Mkuu wa Ofisi yake kutokana na uziwefu wake wa miaka mingi wa masuala ya kiuchumi pamoja na ujuzi wake wa kupambana na mfumuko wa bei nchini humo. Aliongeza kuwa mahusiano yake na Lula sio ya kutafuta nguvu ya kisiasa bali ni mahusiano ya kutaka kujenga nchi pamoja.

"Lula atakuja serikalini kusaidia kazi, tutafanya kazi pamoja kurejesha ukuaji wa uchumi, kuleta utulivu wa fedha na kudhibiti mfumuko wa bei," amesema rais wa Brazil Dilma Rousseff.

Lula ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa Brazil

Brasilien Präsidentin Dilma Rousseff
Picha: picture-alliance/dpa/F. Bizerra Jr.

Uchumi wa Brazil ukiwa unaporomoka na kuwa katika hali mbaya kuwahi kutokea katika kizazi cha hivi karibuni, hasira dhidi ya Rais huyo zinazidi kupanda miongoni mwa wananchi na upinzani, huku uchunguzi wa madai ya rushwa unaohusisha pia kampuni kubwa ya mafuta ya Petrobras ukiwa unatishia kuharibu jina lake.

Kumteua Lula kama Mkuu wa Ofisi yake, ambaye wiki iliyopita alishitakiwa na madai ya kujipatia fedha kwa njia haramu pamoja na udanganyifu ikiwa ni miongoni mwa mambo yanayofanyiwa uchunguzi dhidi yake, kunakosolewa vikali na vyama vya upinzani kama njama ya kumtafutia uungwaji mkono ndani ya baraza la congress dhidi ya kesi yake hiyo itakayoanza kusikilizwa leo hii.

Lula, mwenye umri wa miaka 70, na aliyekuwa kiongozi wa zamani wa chama cha wafanyakazi, wakati wa uongozi wake baina ya mwaka 2003 hadi 2010 uchumi wa Brazil uliimarika, na kuweza kuwainua kutoka kwenye umasikini Wabrazil milioni 40. Hadi sasa amebaki kuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa nchini Brazil.

Hatua ya Rousseff ya kutanganza uteuzi wa kiongozi huyo katika gazeti rasmi la serikali lililochapishwa jana inasemekana itampa Lula kinga dhidi ya mahakama zote isipokuwa mahakama kuu, jambo litakaloweza kuchelewesha mashitaka dhidi yake.

Hakimu wa shirikisho anayeongoza uchunguzi huo amesema katika taarifa ya jana ya mahakama kuhusu mashitika yaliyowasilishwa dhidi ya Lula, kuliwasilishwa mazungumzo ya simu yaliyorekodiwa yanayodhihirisha wakijaribu kuwashawishi waendesha mashitaka na mahakama kumuunga mkono na kumsaidia kiongozi huyo wa zamani.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo