1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rushwa yaziandama siasa za Ujerumani

Admin.WagnerD12 Novemba 2010

Rushwa hazili siasa za dunia ya tatu, bali hata za dunia ya kwanza, ikiwemo Ujerumani.

https://p.dw.com/p/Q6q6
Chansela wa zamani Helmut Kohl, aliyewahi kufikwa na kashfa ya rushwa
Chansela wa zamani Helmut Kohl, aliyewahi kufikwa na kashfa ya rushwaPicha: AP

Kashfa za rushwa hazikutikani katika biashara ya makampuni makubwa tu bali hata katika siasa. Mara nyingi hali hiyo inahusika na maamuzi maalum ya kisiasa kwa manufaa ya makampuni hayo. Wenye kutoa kandarasi hutegemea mara nyingi kupata ruhusa ya miradi ya ujenzi ambayo inazusha mabishano. Orodha ya visa visivyo vya kuridhisha ni ndefu.

Januari mwaka 1993, ilitangazwa kwamba waziri mkuu wa jimbo la Bavaria, Max Streibl, alipokea hongo kutoka kwa wamiliki viwanda wakati alipokuwa waziri wa fedha. Streibl alituhumiwa kuishinikiza wizara ya ulinzi ya serikali kuu iipatie kandarasi kubwa kampuni moja maalum ya Ujerumani inayotengeneza ndege kwa malipo ya likizo mbili kutoka kwa kampuni hiyo ambayo mwenyekiti wake alikuwa rafiki yake, pamoja pia na kuchangia fedha katika mfuko wa chama chake cha CSU.

Pesa: alama ya rushwa
Pesa: alama ya rushwaPicha: picture-alliance/dpa

Mbali na hayo, Streibl anasemekana alitakiwa aingilie kati katika wizara ya utafiti ya serikali kuu na katika taasisi ya kimkoa inayogharimia miradi ya ujenzi mpya ili kumtafutia misaada ya fedha rafiki yake wa utotoni. Hata hivyo, Streibl hakuwa akizijali hapo awali tuhuma hizo.

Kashfa nyengine ya kisiasa iliripuka katika miaka ya '80 kwa jina Kashfa ya Flick. Kashfa hiyo ilihusiana na michango ya siri inayotolewa kwa vyama vya kisiasa. Chanzo cha kashfa ya Flick ni biashara kubwa katika soko la hisa iliyoipatia kampuni hiyo mashuhuri ya Flick kitita cha karibu DM bilioni mbili mnamo mwaka 1975. Kampuni ya Flick ilituma maombi wakati ule katika wizara ya uchumi ya serikali kuu kutaka iruhusiwe isiilipie kodi ya mapato biashara hiyo. Kodi ya mapato ambayo ingebidi ilipwe ingefikia karibu DM bilioni moja.

Waziri wa uchumi wa serikali kuu wakati ule, Hans Friedrichs, na aliyekabidhiwa wadhifa huo baadae, Otto Graf Lambsdorff, wote wa kutoka chama cha kiliberali cha FDP, waliunga mkono biashara hiyo. Mwaka 1981 wachunguzi wa wakwepa kodi walipokagua vitabu vya hesabu vya kampuni hiyo kubwa ya Flick waliona malipo ya fedha zilizotolewa kwa wanasiasa wa vyama vyote vilivyokuwa vikiwakilishwa bungeni wakati huo. Kwa vile majina ya Hans Friderichs na Otto Graf Lambsdorff yalikuwepo miongoni mwa wale waliopokea fedha hizo, ilishukiwa kuwa fedha hizo zilihusika na hongo. Kwa mujibu wa meneja wa kampuni ya Flick, Eberhard von Brauchitsch, fedha hizo zilikuwa mchango uliotolewa kwa chama.

Hatimae Eberhard von Brauchitsch na mawaziri wa zamani wa uchumi, Hans Friderichs na Otto Graf Lambsdorff, walihukumiwa kuisaidi kampuni hiyo kukwepa kulipa kodi. Meneja wa Flick alipewa kifungo cha nje na Friderichs na Lambsdorff walitozwa faini.

Kashfa nyingine ilikikumba chama cha CDU mwishoni mwa miaka ya tisini wakati Helmut Kohl alipokuwa Kansela wa Ujerumani. Kashfa hiyo imepelekea Helmut Kohl kujiuzulu kama mwenyekiti wa heshima wa chama cha CDU.

Mwandishi: Prema Martin/Arne Lichtenberg/ZPR

Mpitiaji: Josephat Charo