1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda: Gacaca zaweka rekodi ya dunia

Admin.WagnerD18 Juni 2012

Wakati mahakama hizo zinafikia ukomo hii leo (18-06-2012) serikali ya Rwanda inasema Gacaca zimepata mafanikio kuliko ilivyotarajiwa.

https://p.dw.com/p/15H6M
Idadi kubwa ya Watutsi walipoteza maisha mwaka 1994 nchini Rwanda.
Idadi kubwa ya Watutsi walipoteza maisha mwaka 1994 nchini Rwanda.Picha: picture-alliance/dpa

Wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, serikali iliyokuwa madarakani wakati huo ilirejea historia yake katika kutafuta suluhu ya changamoto ya upatikanaji wa haki kwa waathirika wa mauaji hayo. Mahakama za kienyeji na mabaraza ya wazee maarufu kama Gacaca zilianzishwa mwaka 2002 na zimekamilisha kesi milioni moja na nusu zinazohusiana na mauaji hayo ya halaiki katika kipindi cha miaka 10.

Hatahivyo, mashirika ya haki za binadamu hayajaridhishwa na namna ambayo mahakama hizo zimeshughulikia baadhi ya kesi , yakisema kwamba hayakutoa hukumu kwa haki.

Dhima kubwa ya Gacaca ni ipi?

Mahakama za Gacaca zilipoanzishwa mwaka 2002, dhumuni lao kuu lilikuwa ni kutoa haki na kuimarisha mapatano miongoni mwa wanajamii ambao wamesambaratishwa kufuatia mauaji hayo.

Takriban watu laki nane, wengi wao wakiwa wa kabila la Kitutsi na Wahutu kiasi waliuwawa katika kipindi cha siku 100, na kwa kutilia maanani ukubwa wa uhalifu uliofanyika, kulikuwa na watu wengi waliokuwa na hatia hali iliyosababisha changamoto kubwa kuamua kesi hizo kwa haki.

Maelfu ya watu waliouwawa walizikwa mjini Kigali.
Maelfu ya watu waliouwawa walizikwa mjini Kigali.Picha: DW

Waziri wa Sheria, Tharcisse Karugarama, anasema mahakama za Gacaca zimetumika kukabiliana na changamoto hiyo, kwa kufanikiwa kusikiliza idadi kubwa ya kesi hizo tena kwa muda mfupi, na hivyo kuweka rekodi ya dunia.

"Sidhani kama kuna mahakama ile duniani iliyotoa hukumu kwa kesi milioni 1.9 katika kipindi cha miaka 10.Kwa hivyo kama mahakama hizi zimefanikiwa kukusanya ushahidi, kutoa hukumu na kuwatia watu hatiani, basi unaweza kusema mahakama za Gacaca zimefanya vizuri kuliko mahakama yoyote ile." anasema Karugarama.

Mahakimu walipatikanaje?

Mahakimu waliokuwa wakiendesha kesi hizo walichaguliwa na watu miongoni mwa jamii, wengi wao kutokana na uadilifu wao. Idadi kubwa ya mahakimu hao hawakuwa na mafunzo yoyote ya kisheria, lakini walipaswa kutoa hukumu katika kesi ambazo ni tata mno.

Katika ripoti yake ya mwaka 20122, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu, Human Rights Watch, lilisema ukosefu wa weledi pamoja na mapungufu mengine yalichangia mahakama hizo za Gacaca kushindwa kufikia viwango vya kimataifa vya utoaji wa hukumu.

Msimamo wa Human Rights Watch

Carina Tertsakian ni mtafiti mkuu wa Kitengo cha Afrika cha shirika la Human Rights Watch na hapa anaeleza "Nafikiri pamoja na nia njema ya dunia, itakuwa ni jambo lisilo sahihi kutegemea watu wasiokuwa na utaalam wowote wa kisheria kushughulikia kesi kama hizo."

Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame.
Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame.Picha: picture-alliance/dpa

Lakini serikali ya Rwanda inadai kwamba kwasababu uhalifu mkubwa ulifanyika waziwazi, wanajamii wangeweza kutoa ushahidi wa uongo na hii ina maana mahakama hizo hazikulazimika kutegemea sheria na miongozo ya kawaida mahali ambapo upande wa utetezi; jambo ambalo kwa mujibu wa Waziri wa Sheria Karugarama ni tafsiri dhaifu ya utoaji wa haki.

"Haihitaji mtu kusomea sheria kuona au kusikia kwamba mtu fulani alifanya jambo hili. Haihitaji mtu kuwa na stashahada ya sheria, haihitaji akili ya ajabu kujua kwamba huu ni ukweli." Anafafanua zaidi Waziri huyu wa Sheria.

Na wakati mahakama hizo zikifikia ukomo wake tarehe 18 mwezi huu, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema utulivu unaoshuhudiwa sasa Rwanda unatokana na nguvu ya serikali, huku maelfu wa watu wakiwa wamekimbilia nchi jirani, wakizikimbia mahakama za Gacaca, ambazo Shirika la Human Rights Watch linasema baadhi ya hukumu zilitolewa kwa kuegemea ugomvi na tofauti za nyuma.

Mwandishi: Daniel Gakuba

Mtafsiri: Ndovie, Pendo Paul

Mhariri:Yusuf Saumu