1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda: Mayatima wa mauwaji ya halaiki kunyimwa haki zao

21 Mei 2015

Mauwaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda mwaka 1994, yalisababisha maelfu ya watoto kuwa mayatima baada ya wazazi wao kuwawa. Mayatima hao inawabidi sasa wapiganie vikali mali walizoachiwa na wazazi wao ambazo ni haki zao.

https://p.dw.com/p/1FTj7
Massenbeerdigung in Gatumba
Picha: picture-alliance/AP Photo

Mauwaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda mwaka 1994, yalisababisha maelfu ya watoto kuwa mayatima. Wengi wao pia walipoteza mali za wazazi wao waliouwawa.Mali hizo ni pamoja na maeneo makubwa ya ardhi ambayo walipokonywa ama na walezi wao au jamaa wa familia zao. Mayatima hao iliwabidi wapiganie vikali mali ambazo ni haki zao.

Nyirandayambaje Agnes mwenye umri wa mika 22 ni msichana pekee katika familia yake aliyenusurika na mauwaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994. Wazee wake na jamaa zake wote waliuwawa. Hili limemuwacha msichana huyo kuwa bila ya wazazi, ndugu au jamaa na kuishi katika mikono ya walezi. Mmoja ya walezi wake ni mwanamke mmoja anaedae kuwa jamaa yake wa mbali. Lakini nia ya kweli ya mwanamke huyu ni kumpokonya Nyirandayambaje urithi wake.

Kwa zaidi ya miaka 21, Nyirandayambaje amekuwa akiishi katika hali ya umasikini na ya kukata tamaa. Lakini sasa amekuwa mmojawapo wa maelfu ya mayatima walopokea fidia ya ardhi walizopokonywa.Ghafla msichana huyo, amekuwa mmiliki wa kipande kikubwa cha ardhi cha hekari 8 kilichopo magharibi mwa Rwanda.

"Nashukuru, nitakachofanya sasa ni kujitahidi kupata bima ya afya na pengine nitakodisha sehemu ndogo ya ardhi yangu ili niweze kujipatia pesa za kuendesha maisha yangu, pia nitanunua nguo maana sina hata nguo za kuvaa," anasema Nyirandayambaje Agnes

Kwa wengi wanamuangalia Nyirandayambaje kama mtu aliyebahatika. Ingawa alikuwa na maisha ya dhiki kwa miaka 21, maisha yake yalibadilika baada ya mfanya biashara mmoja ambae alikuwa anajaribu kununua ardhi - ambayo sasa amerudishiwa mwenyewe Nyirandayambaje - kumtilia shaka muuzaji wa ardhi hiyo na kuamua kuijuulisha mamlaka husika.

Kesi mahakamani bila ya ushahidi wa kutosha

Ruanda Genozid Gedenken 07.04.2014 Paul Kagame
Maadhimisho 2014 ya mauwaji ya halaiki ya RwandaPicha: Reuters

Kwa mujibu wa shirika la manusura wa mauwaji ya halaiki ya Rwanda IBUKA, kuna zaidi ya kesi 300 za mayatima ambao wanapambana kupata urithi waliowachiwa na wazazi wao waliouwawa. Kuna kesi nyingi zinazoendelea mahakamani ambazo zinawapa wasiwasi wengi ya mayatima hao walionusurika na mauwaji ya halaiki.

"Hili ni tatizo lenye umuhimu kwei sisi, kuwepo ardhi ambayo bado hajarejeshewa mmiliki wake. Serikali za mitaa hazijapiga hatua yoyote katika suala hili. Mimi nadhani tatizo kubwa ni wahalifu bado wanakaidi na hili linatokana na kuwa wanakataa kukubali kuwa tatizo hili linatokana na mauwaji ya halaiki," anasema Ndayisaba William, mratibu wa shirika hilo katika wilaya ya Rusizi.

Kwa mujibu wa chama cha IBUKA kesi nyingi ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi, zinatokana na kutokuwapo kwa ushahidi wa kutosha. Mayatima wengi hawana ushahidi wa kutosha unaothibitisha wazazi wao walikuwa wamiliki wa ardhi hizo wanazozidai.

Nyirandayambaje anaamini kuwa lazima fikra za watu zibadilike hasa kwa maafisa wa ngazi za chini, ili ardhi za manusura wa mauwaji ya halaiki zirudishwe kwa wamiliki halali.

Wakati umefika, mayatima kupewa haki zao

Sauti mpya sasa inasikika kupigania matatizo ya mayatima hao na manusura wa mauwaji ya halaiki ya Rwanda ambao wengi wanaishi katika familia zinazoongozwa na watoto. Tume ya taifa ya kupigania haki za binadamu inasema wakati umefika wa kusitisha matatizo ya mayatima hao walionusurika.

"Kwa wale waliowapokonya mayatima walionusurika na mauwaji ya halaiki ardhi zao, wakati umefika wa watoto hao kupewa haki zao. Wakati umefika kwa mayatima hawa kupewa haki juu ya zilizokuwa ardhi za wazazi wao, " anasema Madeline Nirere, rais wa tume ya kutetea haki za binadamu.

Seneti ya Rwanda wameisisitiza serikali ya nchi hio, kuharakiza msaada wa kuwarejeshea ardhi zao mayatima walionusurika na mauwaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994.

Mwandishi: Sella Oneko/Yusra Buwayhid.

Mhariri: Yusuf Saumu