1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sadr awamuru mawaziri wake kujitowa katika serikali ya Iraq.

Mohamed Dahman16 Aprili 2007

Sheikh wa itikadi kali za Kiislam Muqtada al –Sadr leo amewaamuru wafuasi wake kujitowa kwenye serikali ya mseto ya Iraq.Wakatui hatua hiyo haiyumkiniki kuiangusha serikali ya Waziri Mkuu Nouri al Maliki itatowa pigo kubwa kwa kiongozi huyo anayeungwa mkono na Marekani.

https://p.dw.com/p/CHGE
Sheikh Muqtada al Sadr.
Sheikh Muqtada al Sadr.Picha: dpa
Mkuu wa kundi la Al Sadr Nassar al Rubaie akisoma taarifa kutoka kwa kiongozi wao huyo amesema mawaziri wa Al Sadr watajitowa mara moja katika serikali ya Iraq na kuipa serikali nyadhifa hizo sita za mawaziri kwa matumaini kwamba zitatolewa kwa watu huru ambao wanawakilisha matakwa ya wananchi.

Al Sadr na wafuasi wake wamemshutumu al Maliki kwa kushindwa kuunga mkono wito wa kuwepo kwa ratiba ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq.

Waziri Mkuu ametowa taarifa baadae leo hii yenye kusema kwamba kuondolewa kwa wanajeshai wa kimataifa kunahusiana na na kuwa tayari kwa majeshi yao ya ulinzi kuchukuwa uongozi wa usalama katika majimbo yote.

Al Maliki amesema anaukaribisha wito wa Sadr wenye kumtaka kutangaza watu wa kuziba nafasi hizo sita za wafuasi wa Sadr na kuahidi kuendelea kuboresha huduma za serikali.

Al Rubaie pia amewasilisha dai la kutaka kuhamishiwa kwa vikosi vya serikali ya Iraq mahabusu wote wanaoshikiliwa na vikosi vinavyoikalia kwa mabavu Iraq.

Sadr amekuwa haonekani hadharani kwa miezi kadhaa sasa lakini amri yake ya leo ya kuwaondowa wafuasi wake katika serikali inaonyesha kwamba sheikh huyo wa itikadi kali bado ni mtu wa hatari nchini Iraq.

Sheikh huyo wa madhehebu ya Washia ambapo mahala alipo pamekuwa kitendawili tokea mwezi wa Oktoba na ambaye inaelezwa na Marekani kwamba yuko nchini Iran anaendelea kuwa kiongozi mwanamgambo anayetatanisha kabisa na mtu mwenye uwezo katika suala la madaraka katika Iraq ya baada ya kipindi cha Saddam Hussein.

Hatua yake inayokuja inasubiriwa kwa makini wakati wataalamu wakiwa wamegawika iwapo hatua yake ni kurudi nyuma kwa kiongozi huyo mwanamgambo ambaye alitaka kujibadilisha kuwa mwanasiasa au kuwa ni hatua ya ufidhuli ya kuimarisha makao yake ya kizalendo.

Awali akiwa amedaharauliwa na Marekani na serikali ya Iraq mwana huyo wa kiume wa Ayatollah Mkuu aliekuwa akitukuzwa Mohammad Sadiq al Sadr ameonyesha kwamba anaweza kucheza na nguvu za kisiasa liacha ya kuwepo mahala pasipojulikana.

Wafuasi wake wanakanusha kwamba kiongozi wao huyo amejificha na wanadai kwamba anaendelea kuishi na kufanya kazi katika mji wa Najaf ambapo hapo tarehe 9 mwezi wa April alishindwa kujitokeza kwenye maandamano makubwa ya wafuasi wake.

Sadr anaungwa mkono na jeshi la wanamgambo la Mahdi linalokadiriwa kuwa na maelfu ya wapiganaji wanaomtii na wabunge 32 katika bunge la Iraq linalopigwa vita.

Jeshi la Marekani linawashutumu wanamgambo wake kwa kuwauwa Warabu wa madhehebu ya Sunni katika mzozo wa kimadhehebu unaoisibu Iraq.

Wizara ya ulinzi ya Marekani imewaelezea wanamgambo hao kuwa ni tishio moja kuu kabisa dhidi ya utulivu wa Iraq kuliko hata kundi la Al Qaeda.