1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari za ndege ulaya zaanza tena kwa wingi

21 Aprili 2010

Abiria bado wanateseka viwanja vya ndege.

https://p.dw.com/p/N1pN
Ndege zilizosheheni uwanja wa ndege wa Munich.Picha: AP

Misafara ya ndege,barani ulaya , imeanza tena kwa wingi loe baada ya mtafaruku uliosababishwa na volcano ilioripuka nchini Iceland.

Hatahivyo, abiria wengi wangali wanakabiliwa na shida za usafiri katika kipindi hiki ambacho mashirika ya ndege yanajaribu kupambana na kurundikiana kwa abiria na mizigo.Viwanja 5 vya ndege kati ya vyote 16 vya kimataifa vya Ujerumani, vilianza upya safari zao leo na mashirika ya ndege,makampuni yanayounda ndege,Jumuiya ya safari za ndege ulimwenguni (IATA),serikali na wanasayansi,wakipanga kukutana karibuni kuzingatia usalama wa misafara ya ndege inayohusiana na jivu la volcano.

VIWANJA VYA NDEGE:

Vitano kati ya viwanja 16 vya kimataifa nchini Ujerumani vimeanza kazi ya usafiri na wakuu wa viwanja vya ndege wamearifu kiwamba wanatumai kuruhusu ndege zaidi kuruka kutoka anga la Ujerumani baadae hii leo.

"Kutokana na hali ya wingu la jivu,anga katika jiji la Hamburg,Bremen,Hannover,Berlin Tegel na Berlin Schönefeld, linaruhusu usafiri hivi sasa." Shirika la usalama wa anga nchini Ujerumani DFS limesema katika taarifa yake.

Likaongeza kusema kwamba, hali ya hewa jinsi ilivyopambazuka itaruhusu misafara zaidi ya ndege hii leo.Na katika uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi kabisa barani ulaya, Heathrow Airport, mjini London, ndege ya shirika la ndege la Uingereza (British Airways) kutoka Vancouver, Canada, ilitua salama usalimini. Hiyo ilikua ndege ya kwanza kabisa kutua tangu wakuu kuufunga uwanja huo wa ndege kwa safari za ndege wiki iliopita.

ABIRIA:

Mamilioni ya abiria walinasa na wengine bado wamekwama katika viwanja vya ndege mbali mbali ulimwenguni, tangu Ulaya ilipoanza kufunga anga lao kwa safari za ndege hapo April 14 na nyakati za safari za ndege zimeparaganyika baada ya ndege zao nyingi kuambiwa si ruhusa kuruka.

Shirika la ndege la EASY JET likaongeza kusema "kutokana na ukubwa wa mparaganyiko ,itachukua siku nyingi kuanza shughuli za kawaida na yamkini kuawepo hali ya kuchelewa safari."

ITA-Shirika la misafara ya Ndege la Kimataifa, linasema msukosuko huu umeyagharimu mashirika ya ndege dala milioni 200 tena kwa siku.

MKUTANO:

Mashirika ya ndege,viwanda vinavyounda ndege,Jumuiya ya misafara ya ndege Ulimwenguni (IATA) serikali na wataalamu wa sayansi wanapanga kukutana karibuni kuzingatia usalama wa misafara ya ndege inayohusiana na jivu la volcano.

Kuripuka kwa Volcano nchini Iceland, kumepunguka kasi kwa kima cha 80% tangu mwishoni mwa wiki-hii ni kwa muujibu wa taarifa kutoka Reykjavik.Darasa gani walimwengu wamejifunza kutokana msukosuko huu ?

Afisa mmoja wa shirika la ndege asema:

"Kutokana na msukosuko huu, wanaadamu wameweza kutanabahi jinsi masafa yalivyo marefu.Kuwa si kawaida tu kuchukulia unaweza kusafiri hadi km 8000 kwa muda wa masaa 3-4 na kuwa dunia yetu hii ni kubwa."

Athari za msukosuko wa wingu la jivu la volcano katika usafiri ,uchumi na shida za abiria , yadhihirika zitaendelea alao kwa muda fulani.

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman