1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sakata ya maziwa China watoto watatu wafa

Kalyango Siraj17 Septemba 2008

Wanne wakamatwa kutokana na sakata hiyo

https://p.dw.com/p/FJfk
Mtoto mgonjwa anahudumiwa katika hospitali moja nchini China baada ya kunywa maziwa yaliyokuwa na kemikali ya MelaminePicha: AP

Watoto wachanga watatu wamefariki na wengine zaidi ya 150 kupata matatizo ya figo nchini China baada ya kutumia maziwa yaliyokuwa na kemikali aina ya melamine.

Watu wanne wanasemekana kukamatwa kutokana na kuchanganya maziwa na kemikali hiyo.

Taarifa zaidi zinaanza kujitokeza kutokana na kile ambacho kimekuja kujulikana kama sakata ya maziwa ya China.Maziwa hayo ya unga ni ya watoto wachanga.

Sakata hiyo imejulikana baada ya watoto watatu ambao walikunywa maziwa yaliyokuwa na kemikali kufariki huku wengine zaidi ya 6,000 kupata matatizo ya figo.

Katika uchunguzi wao maafisa wa China wamegundua kemikali ya kiviwanda aina ya Melamine ikiwa ndani ya maziwa hayo yanayotengenezwa na viwanda vya maziwa vya China vipatavyo 22.

Kutokana na uchunguzi wa maafisa hao sasa inasemekana watu wanne wamekamatwa kuhusiana na kuchanganya kemikali hiyo katika maziwa. Inadaiwa kuwa walichanganya kemikali ya melamine ili kuipiga jeki lishe ya protini inayopatikana katika maziwa.

Wengi wa watoto waliougua kutokana na kunywa maziwa hayo,inakisiwa waliyatumia katika kipindi cha kati ya miezi mitatu na sita.

Na watoto watatu walikufa kutokana na matatizo ya figo.

Tatizo hilo liligunduliwa na kampuni ya New Zealand ya Fonterra ambayo inamiliki asili mia 43 ya kiwanda cha China cha San Lu ambacho kinasemekana ndicho kilihusika na sakata hiyo.

Maafisa wa serikali ya China wanasema kuwa wakuu wa kiwanda cha San Lu walijua mapema, tangu mwezi Machi mwaka huu, kuwa maziwa yao yamechangwa na kemikali hiyo lakini hawakuchukua hatua madhubuti kujaribu kuonya wananchi ama kuyarejesha maziwa hayo kutoka masoko hadi wiki hii.

Kemikali ya melamine, miongoni mwa mengine, hutumiwa nchini China kwa kuichanganya katika chakula tofauti kinachotumiwa na wanyama.

Inaaminiwa kuwa kemikali hiyo inauwezo wa kupiga jeki lishe ya Protini.

Hata hivyo kemikali hiyo imepigwa marufuku nchini China na Marekani kuwekwa katika chakula.

Makampuni kadhaa kutoka sehemu mbalimbali za dunia yamekuwa yakimiliki viwanda vya maziwa nchini China.Sakata hiyo sasa imeleta wasiwasi katika baadhi ya makampuni hayo.Kampuni moja nchini Denmark imesema kuwa imesitisha uzalishaji wa maziwa ya unga katika kiwanda cha ubia nchini China kutokana na sakata hiyo.

Raia wengi nchini China wamebadili hali yao ya maisha kutokana na matangazo yanayotolewa na kampuni zinazotengeza maziwa ya unga.

Badala ya kuwanyonyesha watoto wao,huwapa maziwa ya unga ama huwanyonyesha mda mfupi na baadae kuwapa maziwa ya unga kupitia chuma.

Watoto zaidi ya 6,000 waliougua kutokana na maziwa haya inadhaniwa walikuwa hawatumii maziwa ya mama.

Wataalamu wengi wamekuwa wakishauri kuwa kumnyonyesha mtoto ndio njia bora ya kumsaidi mtoto kuimarisha mfumo wake wa kinga.Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia watoto la UNICEF linasema kuwa maziwa ya mama husaidia sana kupunguza vifo vya watoto wachanga katika mataifa yanaonukia.

La ajabu ni kuwa makampuni mengi ya kimataifa yanayotengeneza maziwa ya unga kama vile Nestle,yanasema yanaunga mkono hatua ya kumnyonyesha mtoto.