1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Salah ndiye mchezaji bora wa Afrika 2017.

Lilian Mtono
5 Januari 2018

Mohamed Salah ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika, katika hafla iliyofanyika mjini Accra, akiwa ni raia wa kwanza wa Misri kushinda tuzo hiyo tangu Mahmoud Khatib aliyeshinda mnamo mwaka 1983.

https://p.dw.com/p/2qOXF
Ghana Fußballer Mohamed Salah in Accra
Picha: Getty Images/AFP/U. Ekpei

Mohamed Salah ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa shirikisho la kandanda barani Afrika,(CAF) katika hafla iliyofanyika kwenye mji mkuu wa Ghana, Accra jana Alhamisi, akiwa ni raia wa kwanza wa Misri kushinda tuzo hiyo tangu Mahmoud Khatib aliyeshinda mnamo mwaka 1983.

Mshambuliaji huyo machachari wa Liverpool inayoshiriki ligi kuu ya kandanda ya England, PL amefunga magoli 23 katika mechi 29 kwenye mashindano yote ya msimu huu ya ligi hiyo, akitokea AS Roma ya Italia katika kipindi cha uhamisho cha majira ya joto. Salah pia aliisaidia Misri, ambayo mwaka jana ilimaliza katika nafasi ya pili, nyuma ya Cameroon katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika na kupata nafasi ya kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kombe la dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990.

Salah ambaye ni raia wa Misri alifunga bao la penati katika mechi ya kufuzu kuingia kwenye michuano ya kombe la dunia, na kuiondoa Congo Brazaville katika mechi iliyochezwa mjini Alexandria.

Fußball, Premier League, Liverpool - Southampton
Mohamed Salah akipongezwa na kocha wake Jurgen Klopp katika mechi kati ya Liverpool na Southampton Picha: picture-alliance/Citypress24

Mchezaji mwenzake kutoka Liverpool, Sadio Mane wa Senegal alikuwa wa pili na mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2015 na raia wa Gabon anayechezea Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang alishinda nafasi ya tatu, baada ya mchujo wa orodha ya wachezaji 30. 

Makocha wa timu za taifa, maafisa wa shirikisho la soka Barani Africa, CAF, waandishi wa habari na umma, walishirikishwa katika kuwapigia kura washindi. Salah, anachukua tuzo hiyo ya juu zaidi ya mtu mmojammoja ya CAF kutoka kwa mshindi wa mwaka jana, raia wa Algeria Riyad Mahrez anayechezea Leicester City. 

Tuzo nyingine zilikwenda kwa mchezaji bora wa soka wa mwaka kwa upande wa wanawake, Asisat Oshoala wa Nigeria na mchezaji chipukizi wa mwaka Patson Daka wa Zambia. 

Kocha, raia wa Argentina anayeifundisha Misri, Hector Cuper alitajwa kuwa kocha bora wa mwaka na tuzo nyingine zilienda kwa timu ya taifa ya Misri, timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini na klabu ya Wydad Casablanca.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Bruce Amani