1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SALUM ABDALLAH ATABAKIA KIJANA MILELE

Christopher Buke28 Aprili 2007

Nyimbo zake zingali zikichezwa hadi hivi leo

https://p.dw.com/p/CHcG

Sidhani kama nitakosea kusema kuwa Salum Abdallah atabakia kijana milele. Mara ya kwanza kuvutiwa na mwimbaji huyu ilikuwa baada ya kusikia wimbo wake ukichezwa redioni.wimbo huo unaitwa “ Nalia nasikitika”.

Wimbo huu wa Salum Abadallah ni moja ya nyimbo nyingi alizoziimba wakati wa uhai wake kabla ya kuaga dunia mwaka 1965 katika ajali ya gari.

Kwa hakika nyimbo zake zitakumbukwa daima dawamu maadhali dunia hii ingalipo. Ndio maana wajanja wengi wamezihifadhi na waziuza, baadhi kupatikana katika mtandao wa Internet.

Taklibani nyimbo zote alizozitunga msanii huyu zina vuta hisia kali. Inategemea wewe msikilizaji yamekusibu yepi, au unafurahishwa na nini. Basi katika albamu au kanda ya Salum Abadallah ikichezwa haidhuru kuna wimbo utaomba urudiwe kuchezwa au kama wengine walivyokuwa wakisema wakati ule once more(yaani uweke tena wimbo huo).

Hapo kama yupo anayefahamu mambo huelewa wimbo huo umegusa maswahibu yako. Lakini kingine ambacho huenda kilifanya nyimbo za msanii huyu zipendwe sana, ni kutokana na staili ya utunzi wake. Alikuwa akitunga nyimbo fupi fupi lakini zenye ujumbe wa moja kwa moja. Wimbo unaimbwa beti mbili tu na kibwagizo unaisha ungali mtamu.

Ni machache sana, yanajulikana juu ya historia ya mwanamuziki huyu. Ni wachache wamehangaisha vichwa vyao kuandika habari zake ikilinganishwa na jinsi ambavyo wengi wanaochuma pesa kutoka nyimbo zake na hivyo ndivyo dunia ilivyo.

Ni kutokana na ombwe hilo pamoja na utashi wa kutaka kujua mengi juu ya Salum Abdallah, na kumuenzi mwanamuziki huyu vilivyo nisukuma nisafiri hadi mjini Morogoro mji aliozaliwa, kukulia na kumalizia maisha yake.

Tena mji huu kusema kweli umezalisha wanamuziki wengi enzi hizo kama mwenyewe Salum Abadallah, Juma Kilaza, Mbaraka Mwishehe na wengine wengi. Halafu watu wasivyo na dogo wakadiriki kuuita Morogoro kuwa ni Mji kasoro bahari. Mimi sishangai hata kidogo maana ndivyo dunia ilivyo.

Hata kama ina kasoro ya bahari alau Morogoro imejijengea umaarufu mkubwa kutokana na mambo mengi. Mojawapo ni hawa wanamuziki walioiinua Tanzania katika safu ya muziki.

Na ndio maana sikupata shida kujua nyumbani kwao na Salum Abadallah pamoja na wanamuziki kadha wa kadha mjini Morogoro. Kwenye kijiwe kimoja tu niliomba kuelekezwa sehemu hiyo na matokeo yake nikapewa mtu tena mzima na kwa hiari yake mwenyewe na akanipeleka.

Hii inadhihirisha ni kiasi gani mwanamuziki huyo alivyopendwa. “ Unakwenda kwao na Salum Abdallah? ntakupeleka” aliniambia Bwana Muhamed Hashim Mkazi wa mjini Morogoro.

“ Nyumba ile pale” alinionyesha nyumba kwa ishara ya kidole, baada ya kukatiza karibu mitaa mitatu na kwa vile nilimkuta akifanya kazi yake alirudi kuendele na mahangaiko ya kuitafutia familia yake mkate.

Kwa nasibu mtu aliyekuja kunifungulia mlango ni dada yake na Salum Abdalah. Bi Jamila Abadallah. Ni Bibi mcheshi, Mwenye heba, anaongea taratibu na kwa kujiamini. Bibi huyu hivi sasa ana umri wa miaka 65.

Nikasabahi, nikajitambulisha na kumwambia shida yangu ya kujua machache kuhusu Kaka yake. Bi Jamila angali akikumbuka sana wema na roho nzuri aliyokuwa nayo ndogo wake.

“Ama heba yake kwa wakazi wa Morogoro ilikuwa nzuri sana na alikuwa mtu mkarimu sana. Ilikuwa haiwezekani akija mtu labda ana shida akamrudisha nyuma! Ni lazima amsaidie. Kwa hiyo alipendwa sana sana sana! Hata siku aliyofariki ilikuwa kwa kweli eneo hili lote lilijaa watu hapa nje. Walikuja kuzika ilikuwa haijatokea sijui kama rekodi hiyo ilitokea baada ya miaka katika mazishi yake”.

Lakini hapa lazima mtu ajiulize, je mwanamziki huyu alipendwa kiasi hiki, na kuwa maarufu namna hiyo kutokana tu na ukarimu wake kwa watu? Ndio lakini kwa sehemu kidogo, zaidi alikuwa maarufu kutokana na muziki wake. Ulikuwa ukichoma hadi rohoni.

Mzee Kassim Mapili ni mojawapo wa wanamuziki wakongwe hapa nchini. Anakubaliana na hoja hii. Anasema Salum Abadallah alipendwa sana hadi nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na utamu wa muziki wake.

“Lakini amekufa angali bado kijana, na alipendwa kwa sababu maziko yale pale, walikuja watu mpaka hata kutoka Mombasa, sababu tungo zake na mahazi yake, yalikuwa yanaambatana, yalikuwa yanaingia kote-kote, ukisikia tungo wewe unayependa mziki wa dansi utapenda, unayependa mziki wa taarabu kwa sababu ilikuwa kama anaghani, zile lafidhi zake”, anasisitiza Mzee Mapili.

Mojawapo ya nyimbo ambazo Salum Abadallah ameghani kama vile utadhani ataka kuimba taarabu ni ule wa “ ngoma iku huku”, huku wapi sijui lakini baadhi ya beti za wimbo huo zinaselelea zikisema.

Mpenzi wangu ngai eeeeh, ngai eeh

fika uone kisangani eeh

mpenzi wangu ngai eeh ngai eeh

ngoma iko huku

njoo ufurahi ngoma iko huku, cubana na marimba aah kisangani, ukitaka rumba rumba iko huku, ukitaka chacha chacha liko huku, ukitaka samba samba liko huku, cubana na marimba kisangani.

Ukitaka twisti twisti liko huku cubana marimba kisangani”. Na kadhalika na kadhalika.

Kwa hakika hivi ni vionjo ambavyo vilitikisa sana nyoyo za washabiki wake, na wapenzi wa muziki. Kila mmoja kwa maswahibu yake.

Mfano Bi Jamila Abdallah anasema wimbo ambao kwa miaka yote hiyo ungali ukimliwaza na anaukumbuka sana ni ule wa “walimwengu”.

Hebu tuone baadhi ya maneno yaliyo kwenye beti za wimbo huo.

Nasikitika mwenzenu,

kwa majonzi ya moyoni,

ulimwengu wanipiga

maisha siyatamani,

Kiitikio:

pole pole ndio dunia

pole pole ndio dunia.

Ubeti wa pili

Wazazi walinitupa

miaka mingi kupita

ndugu tumetawanyika

wala hatutambuani

Kama ningeliushika

wazazi wao wasia

siku walipotoweka

singekuwa adhabuni.

Hivi ukitathmini maneno yaliyo katika beti hizi unaweza ujue angalau ni yapi yanayorandana na wimbo huo hasa ukilinganisha na wimbo ambao mimi mwenyewe ulinigusa, wenye beti zisemazo.

Nalia nasikitika

mchozi yanidondoka

mpenzi wangu kanitoka

kaniachia makiwa

Kibwagizo:

Mpenzi we nyamaza kulia

hiyo ndio hali ya dunia.

Kwa mifano hii miwili nyimbo za mwimbaji mmoja, lakini zinawagusa watu tofauti wenye jinsia tofauti lika tofauti na kwa maswahibu tofauti. Huyo ndiye Salum Abadallah.

Kwa Salum Abdallah muziki haikuwa zaidi sehemu ya kupata ajira au kipato, kwake ilikuwa Burudani na kukidhi kiu ya wasikilizaji wake, kuelimisha jamii, na kuinua sifa za taifa lake. Yeye alikuwa mfanya biashara kama alivyoniambia Dada yake.

“ alikuwa na shughuli zingine akifanya alikuwa na magari akifanya kazi za biashara, na hata hiyo ajali ilimkuta kwa sababu alikuja driver kumfahamisha kwamba gari moja imeharibika huko, kwa hiyo ilibidi atoke na gari nyingine pamoja na driver ndio njiani kwa bahati mbaya kapata accident (ajali). Alikuwa na shughuli zingine akifanya”.

Maskini kifo kikamchukua katika wakati ambapo hakingepaswa kufanya hivyo. Watu wengi walikuwa wangali wakimpenda. “ bahati mbaya alifariki kijana sana ndio kwanza alikuwa ameoa na alikuwa hajapata mtoto manake kifo chake kilikuwa cha accident”, ananiambia Bi Jamila kwa masikitiko.

Ama kwa hakika nyimbo Za Salum Abadallah ziliyakuna hata makundi ya kijamii mfano kama wanawake. Sidhani kuna mwanamke atakaekuja kuchukizwa na wimbo wa mwanamuziki huyu akiwasifu wanawake wa Tanzania pale aliponadi.

“ wanawake, wa Tanzania, wazuri sana

ukisema naye anajibu, hasante sana.

Akikupa kitu husema tafadhali Bwana

Akishika jembe hulima sana, vizuri sana

wanawake siku hizi warembo sana, warembo sana aah”. Na kadhalika na kadhalika.

Nani atapinga kuwa wanawake wa Tanzania sio wazuri sana? Ama apinge kuwa wakishika jembe hawalimi sana? Aende vijijini aone wamama wanavyofanya kazi. Haidhuru mtu anaweza kushupalia hili la kuwa akikupa kitu anasema tafadhali Bwana, hata mimi sijui kama wote wanasema tafadhali Bwana lakini kweli wanawake wa Tanzania ni wazuri sana.

Lakini kwa nini Mwanamuziki huyu akawa na kipawa cha namna hii, kutoa nyimbo zenye mvuto kiasi hiki? Dada yake anasema kipawa hiki kilionekana kwa Salum Abadallah tangu akiwa kijana mdogo.

“Tangu alipokuwa kijana mawazo yake na fikra zake zote zilikuwa kwenye mziki, kwa hiyo alianza kushughulika na mambo ya muziki akipiga piga mziki” anasisitiza Bi Jamila Abdallah.

Sikufahamu baadhi ya mambo kama vile nani alimfundisha mziki Salum Abadallah lakini ningali nikiyafuatilia. Lakini hata dada yake Bi Jamila anasema mengi pia hayajui.

“ mimi siyajua kwa sababu unajua mambo ya muziki ilikuwa yeye ndiyo yapo ndani ya fikra zake sisi tulikuwa, mimi nilikuwa nimekwisha olewa nipo sehemu nyingine lakini najua tu kwamba mwenyewe alikuwa na kipaji hicho, alikuwa na kipaji sana cha muziki na akitunga mwenyewe nyimbo na alikuwa ana uwezo kidogo akinunua vile vyombo pia vya muziki, akishirikiana na wenziwe ilikuwa ni bendi maalumu ikiitwa Cuban Marimba. Basi walikuwa wakiendelea na muziki bahati nzuri muziki wake ukapendwa, na watu wakaupenda sana na sifa yake ndo ikawa kubwa sana hapa nchini Tanzania”.

Lakini kwa upande wake Bwana Muhamed Hashim mzee mmoja mjini Morogoro ambaye anafahamu mengi kuwahusu hawa wanamuziki wa zamani anadhani Salum Abadallah “ilikuwa kama kipaji alichopewa na Mwenyezi MUNGU”.

Hata pale nilipomtaka dada yake aseme macheche seheumu ya kumuenzi mdogo wake hakusita kutoa wito kwa vijana wanamuziki wa sasa, waige mziki wa kaka yake.

“ kwa ajiri ya kumbukumbu ya kaka yangu natoa nasaha kwamba ingekuwa vizuri hawa vijana wa sasa nao wangekuwa labda wangekuwa wanaendeleza ule mziki uliokuwa ukiendelezwa na marehemu kwa sababu ulikuwa ukipendwa na ukionekana kama una utanzania Tanzania hivi”.

Kweli mziki wa Salum Abadalah ulikuwa sio tu na ‘utanzania Tanzania’ bali hata ‘uafrika uafrika’ hivi. Ndio maana baadhi ya nyimbo zake zililenga kulitukuza taifa na badhi ya mataifa ya kiafarika pamoja na vita vya ukombozi wa nchi kadhaa za kiafrika.

Mojawapo ya nyimbo hizi ni huu hapa:

“twafurahia mama muungano, mheshimiwa mwalimu Nyerere, sifa zako zimejaa tele, wananchi twapiga vigere gere, wewe ndiwe baba wa taifa mwenye wingi wa kila sifa, Tanzania umeipa sifa”.

Ama kwa hakikia mziki wake ulipendwa na kutapakaa katika nchi nyingi za kiafrika na hata zile za ulaya. Huenda ikawa ndio maana mwenyewe akaja kuteremka na kibao kingine kilichokuwa kikiinadi bendi yake chenye maneno.

“ Cuban marimba nani asiyeijua, Tanganyika ndiyo iliyoanza jina kutoa, Kenya na Uganda Kongo wanaitambua, kwa nyimbo zake nzuri na maneno yenye murua”.

Na pengine ni maneno hayo yenye murua ambayo yamezifanya nyimbo zake zisalie kwenye chati hadi hivi leo. Na ndio maana nikasema kuwa Hakika Salum Abadallah atasalia kijana Milele.

Mwisho.