1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Salva Kiir: Mjadala wa kitaifa utamaliza vita Sudan Kusini

Iddi Ssessanga
24 Agosti 2017

Miaka minne ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, maelfu wameuawa, wakimbizi milioni mbili. Sudan Kusini ni taifa lililofeli. Katika mahojiano na DW, rais wa Sudan Kusini Salva Kiir azunguzia hali inayoendelea nchini mwake.

https://p.dw.com/p/2imYw
DW Interview mit Salva Kiir Mayardit, Präsident Südsudan
Picha: DW/A. Kriesch

Ni takriban miaka minne sasa tangu Sudan Kusini ilipotumbukia katika mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe. Juhudi kadhaa zimefanyika kuutatua mgogoro huo, zikiwemo za kikanda na kimataifa. Juhudi za karibuni zaidi ni kuanzishwa kwa mdahalo wa ndani ya Sudan Kusini yenyewe.

Rais Salva Kiir anasema ana imani juhudi hizi mpya zatafanikiwa kuutanzua mkwamo Sudan Kusini, kwa sababu watu walio na manung'uniko ambayo hayakushughulikiwa katika makubaliano ya awali ya amani, wanaweza kutumia fursa ya mjadala huo wa kitaifa kuelezea manung'uniko yao yaweze kuzingatiwa katika maazimio ya kamati ya majadiliano na pia wakati wa kuundwa kwa serikali huko mbeleni.

'Machar siyo tishio tena kwa serikali'

Kuhusu ushiriki wa makamu wake wa zamani Riek Machar katika mchakato huo mpya, Kiir amesema kanda nzima haimuhitaji Machar kwa sababu kila akirudi anazusha hali ya kuirudisha nchi hiyo kwenye vita. Machar yuko nchini Afrika Kusini ambako Kiir amesema anaishi katika nyumba ya wageni lakini haruhusiwi kutoka nje wala kuwatembelea watu.

Südsudan Riek Machar Rebellenführer
Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar, alieko uhamishoni nchini Afrika Kusini kwa sasa.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Ayene

Rais Kiir alikanusha hoja ya DW kwamba makamu wake huyo wa zamani yuko chini kifungo cha nyumbani. Kuhusu swali la iwapo Machar bado ni tishio kwa serikali, rais Kiir alisema, "siyo tishio kwa serikali, lakini anasababisha tu machafuko, anawapigia simu wafuasi wake hapa ambao anajua walipo, na hao ndiyo wanaedelea kusababisha matatizo, anawaambia waendelee kupigana na kutokubali amani. Na hivyo mtu kama huyu hana uwezo wa kuongoza, na hana moyo wa umoja, anapenda tu watu wauawe kila siku."

Kiir alizungumzia pia usalama wa ndani kufuatia matamshi yanayotolewa na wakosoaji wake kwamba amejikita tu katika mji mkuu Juba na kwamba yeye ndiyo amekuwa meya wa mji huo kwa sababu hawezi tena kuondoka kwenda mahala kwingine kwa kuhofia usalama wake, akisema alitoka na kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais wa Rwanda Paul Kagame Ijumaa iliyopita.

Ukiukwaji wa haki za binadamu

Kuhusu tuhuma za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini, unaodaiwa kufanywa pia na wanajeshi watiifuku kwake, rais Kiir alisema siyo kweli kwamba vikosi vya serikali ndiyo vinatenda uhalifu huo. "Watu wengi nchini Sudan Kusini wana silaha, na watu hao wamejipatia pia sare sawa na za jeshi la serikali kwa njia zao, na wanaweza kujifanya kama wanajeshi wa serikali, katika muundo wowote, iwe jeshi la ulinzi, polisi au askari magereza na kisha kutenda unyama kama huo," alisema rais Kiir.

Kiir alisema lakini, iwapo wanajeshi wa serikali watajihusisha katika vitendo vya uhalifu wanafikishwa mbele ya sheria, ingawa katika maeneo mengi ya vijijini nchini humo, ni vigumu kwa raia kuweza kwenda hata katika vituo vya polisi na kuripoti matukio hasa yanayowahusu walinda usalama.  Kuhusu swali hili Kiir alisema, "pengine unaweza kuwa unajua zaidi yangu, lakini nnachojua mimi kama kiongozi wa nchi ni kwamba siyo."

Uchumi wa Sudan Kusini unaotegemea zaidi mafuta umetumbukia katika mdororo mkubwa kiasi kwamba serikali imekosa fedha za kuwalipam watumishi waumma wakiwemo hata wanajeshi kwa muda wa miezi minne sasa. Rais Kiir anasema hilo haliwezi kuchochea mgogoro, lakini alilaumu hali hiyo kwa vita na kusema huwezi kujenga uchumi huku unapigana vita. Alisema serikali itawalipa watumishi na wanajeshi mishahara yao pale itakapopata fedha, bila kutaja muda maalumu na wapi pesa hizo zitapatikana, lakini akifananisha hali ya sasa na wakati wa mapambano ya kuwania uhuru wa nchi hiyo ambapo walijitolea bila kulipwa malipo yoyote.

DW Interview mit Salva Kiir Mayardit, Präsident Südsudan
Rais Kiir akiwa na mwandishi wa DW Adrian Kriesch ofisni kwake mjini Juba.Picha: DW/A. Kriesch

Malumbano kuhusu kikosi cha kanda cha kulinda amani

Kuhusu mgogoro kati ya serikali yake na Umoja wa Mataifa kutokana na kuletwa kikosi cha kanda cha ulinzi wa amani ambacho serikali ya Sudan Kusini inakipinga, rais Kiir alisema kilichokubaliwa na viongozi wa kanda hiyo siyo kilichotekelezwa na kukosoa pia kikosi hicho kuitwa cha kanda kwa sababu kinajumlisha wanajeshi ambao hawatoki katika kanda bali wengi wao hutoka nje ya bara la Afrika, akisisitza kuwa wanajeshi hao hawana kazi nchini Sudan Kusini licha ya ukweli kwamba wamewaruhusu kuwepo na kwamba mvutano uliopo utasuluhishwa kwa njia muafaka.

Salva Kiir ameiongoza Sudan Kusini tangu 2011, na ni miongoni mwa waasisi wa vuguvugu la waasi la SPLM, ambalo lilipigana vita vya kikatili vya uhuru kutoka kwa Sudan kati ya mwaka 1983 na 2005, kabla ya nchi hiyo kutangaza uhuru wake mwaka 2011. Taifa hilo lilitumbukia katika mgogoro wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo makundi tofauti ya waasi yanapambana na vikosi vya serikali. Makundi ya haki za binadamu na Umoja wa Mataifa yanazilaumu pande zote katika mgogoro huo kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Mwaka 2016 katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alionya juu ya kutokea mauaji ya kimbari nchini humo.

Mahojiano: Adrian Krisch (HA Afrika)
Ripoti: Iddi Ssessanga
Mhariri: Mohammed Khelef