1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sanders, Trump washinda jimbo la West Virginia

11 Mei 2016

Mgombea wa urais wa Democratic Bernie Sanders amempiku Hillary Clinton katika uchaguzi wa mchujo katika jimbo la West Virginia, wakati Donald Trump amenyakua majimbo mawili zaidi

https://p.dw.com/p/1IlRn
USA Demokraten Wahlkampf Kalifornien - Bernie Sanders
Picha: Getty Images/J. Sullivan

Kwa upande wa Republican, mgombea aliyebaki Donald Trump amenyakua majimbo mawili zaidi.

Bernie Sanders, Seneta wa Vermont mwenye umri wa miaka 74 ameshinda jimbo la West Virginia na kuyaweka hai matumaini yake dhidi ya mpinzani wake Hillary Clinton. Licha ya kushindwa, Clinton bado anapigiwa upatu kuwa mgombea atakayekiwakilisha chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Novemba 8.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara mjini Salem, katika jimbo la Oregon, ambako Wademocrat watapiga kura wiki ijayo, Sanders alikiri kuwa kampeni yake ingali inakabiliwa na mlima mkubwa "Kwa ushindi wetu usiku huu jimboni West Virginia, sasa tumeshinda chaguzi za awali na mchujo katika majimbo 19, na acha niwe wazi, tupo katika kampeni hii kushinda tikiti ya Democratic".

Amesema watapambana mpaka kura ya mwisho katika majimbo ya Oregon, Kentucky, California, North Dakota na South Dakota. Sanders alishinda wiki iliyopita katika jimbo la Indiana, wakati Clinton akipata ushindi mdogo Jumamosi katika kisiwa cha Pasifiki cha Guam ambacho ni himaya ya Marekani.

Donald Trump Geste Siegesgeste
Sanders anasema sasa kibarua kilichopo ni kwa Wademocrat kumwangusha TrumpPicha: Getty Images/J. J. Mitchell

Ili kupata tikiti ya Democratic, Clinton ana wajumbe 1,700, ikiwa ni 300 zaidi ya Sanders. Ili kuteuliwa, mgombea atahitaji wingi wa kura, au wajumbe 2,383. Clinton anatarajiwa kushinda idadi kubwa ya wajumbe maalum 719 – ambao wengi huwa ni maafisa waliochaguliwa na watu wa ndani ya chama – ambayo itamhakikishia ushindi katika mkutano mkuu wa chama mwezi Julai mjini Philadelphia.

Sanders anatumai kujiimarisha kwa kupata ushindi katika majimbo yajayo yakiwemo Kentucky na Oregon mnamo Mei 17. Wagombea wote pia wataangazia uchaguzi wa Juni 7 ambapo wajumbe maakum 700 watashindaniwa, wakiwemo 475 jimboni California ambako Sanders ameelekeza juhudi zake. Na sasa seneta huyo anasema kazi sasa ni kwa chama kujipanga namna ya kumwangusha Trump "wito wetu kwa wajumbe wa Democratic ambao watakusanyika Philadelphia ni kuwa wakati tuna tofauti nyingi na Hillary Clinton, kuna jambo moja tunalokubaliana, nalo ni: lazima tumshinde Donald Trump".

Katika upande wa Republican, mfanyabiashara bilionea wa Manhattan Donald Trump mwenye umri wa miaka 64 ndiye mgombea pekee anayetarajiwa kupewa tikiti baada ya wapinzani wake wawili kujiondoa kinyang'anyironi wiki moja iliyopita.

Ushindi wa Trump katika majimbo ya Nebraska na West Virginia umemsogeza karibu kabisa na nafasi ya kupata kura za wajumbe 1,237 anaohitaji ili kutangazwa kuwa mgombea wa Republican katika mkutano mkuu wa chama hicho mwezi Julai

Sasa anaangazia macho yake kwenye uchaguzi mkuu, na tayari ameanza kumtafuta mgombea mwenza. Anasema ameunda orodha ya watu watano au sita ambao wana ujuzi wa kisheria mjini Washington. Trump anatarajiwa kukutana na Spika wa Bunge la Marekani Paul Ryan mjini Washington kesho Alhamisi baada ya Ryan kusema wiki iliyopita kuwa hayuko tayari kumuunga mkono Trump.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/RTR/DPA
Mhariri: Josephat Charo